NA WILLIAM SHECHAMBO
WAINGEREZA wakisema ‘days are numberd’, sisi kwa lugha yetu tamu ya Kiswahili tunaweza
kusema siku zinahesabika kwa Watanzania kwenda kwenye shughuli muhimu ya
kupigakura za kumchagua Rais wa Tanzania, wabunge majimboni na madiwani wa kata
husika.
Ni jukumu zito linalohitaji akili tulivu, busara na
uzalendo mkubwa utakaomwezesha mpigakura kufikiria tulikotoka, tulipo na
tunakoelekea kwenye suala zima la maendeleo ya taifa katika sekta zote. Tukio
hili linatungoja sote Oktoba 25, mwaka huu (zimesalia siku 46 tu).
Licha ya kwamba umeshakuwa wimbo, bado ninawiwa kuitumia
nafasi hii kusisitiza Watanzania wenzangu kuachana na mikumbo ya kisiasa isiyo
na tija kwa maendeleo ya taifa hili lenye maendeleo makubwa yanayotusubiri
miaka michache ijayo.
Turudi nyuma kipindi tukiwa darasani, jambo linalofanya
nimkumbuke mwalimu wangu aliyenifundisha msamiati unaoitwa kwa lugha ya kigeni
crowd/mob psychology; Alisema maana nzuri ya msamiati huo inaelezewa na
wataalamu wa saikolojia ya jamii.
Aliwataja wanasaikolojia kadhaa, lakini ninaikumbuka
tafsiri ya Gustave Le Bon, Mfaransa aliyefanya tafiti mbalimbali za masuala ya
saikolojia ya watu, ambaye alisema ni tabia ya mtu kufuata anachoona wengi
wanakifuata mahali alipo.
Alieleza kuwa kitendo cha mtu kufuata mkumbo ni kutokana
na kupungua kwa uwezo binafsi wa kujiongoza na kufuata anachokiamini, hivyo ni
sawa na ugonjwa wa kuambukiza na kutokana na tafiti zake Gustave Le Bon, alisema
mwisho wa wale wanaofuata mkumbo ni mbaya kwa sababu hawakujua kile walichokuwa
wakikifanya.
Unaweza kujiuliza kwanini nimekulazimisha kurudi
darasani kujifunza kuhusu masuala ya mikumbo kama ilivyoelezwa na wataalamu wa
saikolojia ya watu; maana yangu ni kukuleta karibu unielewe zaidi juu ya
kilichonisukuma kuandika hoja hii leo.
Siasa za Tanzania zimeingiwa na hili jambo baya kabisa
kwa mustakabali wa taifa letu. Mikumbo kwenye maeneo mbalimbali huwatesa watu
wasio na hatia na kusababisha vilio vya kusaga meno mara matokeo ya mkumbo huo
yanapokuja. Mfano halisi ni migomo shuleni na kazini.
Kwa namna moja au nyingine ni wazi utakuwa umekutana na
moja ya machungu ya kufuata mkumbo na kama jibu ni ndio, basi unapaswa kurudi
nyuma na kujiuliza nafasi yako ni ipi na namna gani utatumia nafasi hiyo
kuzungumza na Watanzania hasa vijana juu ya athari za mkumbo.
Baada ya kuzungumza na watu mbalimbali, matokeo
niliyoyapata ni kwamba baadhi ya Watanzania wamekosa uzalendo kwa kujihusisha
na siasa chafu zinazoendelea kufanywa na vyama vya upinzani nchini hasa vile
vilivyoko chini ya genge linalojiita UKAWA.
Siasa zao zimejaa hila, ulaghai na kila aina ya uchafu?
Inasikitisha kwasababu vijana wamekuwa ngazi ya wanasiasa hao kutaka kupata
madaraka serikalini huku wakiwa hawana chembe ya malengo yanayoweza kusemwa
kuwa ni madhubuti kwa maendeleo ya taifa hili.
Hivi hatujiulizi kwanini wanatufanyia maigizo
majukwaani? Watu wanafuata mkumbo kwa kuzungumza kwa ghadhabu kutetea viongozi
hao kuwa wako sahihi kwa wanalolifanya huku wakijua kabisa kuwa hawako sahihi.
Siasa za Tanzania yetu watu wanazifanya maigizo, na bado
watu tunawaunga mkono. Kweli hii ni sahihi? Tunaitendea haki nchi hii
iliyowekewa misingi imara na waasisi wetu? Hapana, umefika wakati turudi kwenye
akili zetu. Tusiwe kama vile tumerogwa.
Tanzania ni nchi ambayo kimataifa inafahamika kama
kisiwa cha amani. Tunapaswa kuendeleza hadhi hii kwa kuendelea kuipa ridhaa CCM
ambayo ndicho chama chenye ilani imara yenye dhamira ya dhati kwa maendeleo ya
taifa hili.
Watanzania leo hii wamekuwa kama watazamaji kwenye
ukumbi wa maigizo. Watu mbalimbali wanatumiwa na wanasiasa uchwara mpaka
viongozi wa dini kuwasafishia njia ya tamaa ya madaraka wanasiasa hao.
Zipo dalili nyingi mno ambazo Watanzania tunatakiwa kuzizingatia
na kutozipuuza ili kuiokoa nchi hii kwenda kwenye mikono ya wasiostahili;
lakini kama nilivyosema kwenye kiini cha hoja hii, watu wanafahamu na wanaziona,
lakini wanafuata mkumbo.
Vitabu vya dini vimeeleza kuwa mwanamke mpumbavu
huibomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe. Watanzania tunatakiwa kufikiria
kwa kina kwenye kufanya maamuzi katika uchaguzi wa mwaka huu. Tusije tukawa
wapumbavu baadae kwa kuiharibu nchi yetu kutokana na mkumbo usiokuwa na maana.
Yapo mataifa yameshaanza kutoa udenda kwa matamanio ya
kutuvuruga Watanzania, kisha waje na kuchukua waliyokuwa wakiyatamani kwa miaka
mingi tangu awamu ya kwanza ya taifa hili, baada ya uhuru kutokana na utajiri
wa rasilimali tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu.
Hili halipingiki. Kila kiongozi wa kisiasa unayemwona
anatumia kila njia kufika anapopataka, fahamu kuwa yuko mtu anamshika mkono kwa
makubaliano maalumu ambayo mwisho wa siku wote watahitaji kunufaika.
Binafsi katu sikubali kuwa miongoni mwa watakaolia kwa
kusaga meno baada ya wasiostahili kufanikiwa kuwalaghai wafuata mkumbo kwa
tamaa ya wachache. Sikubali na sitakuja kukubali hata miaka 30 ijayo kwasababu
tulipo sasa ni mikono salama.
Nakamilisha hoja yangu kwa kushauri kuwa, haya maigizo
ni vyema tuyatizame kwa kujifurahisha na kama darasa la kuwasoma zaidi
wanasiasa hao uchwara ambao wanaiona nchi hii kama ukoo au kabila fulani na wao
wanahitaji kuwa machifu kisha tuwapuuze Oktoba 25. Lakini tukumbuke ‘days are
numbered’
MUNGU Ibariki Tanzania, MUNGU bariki uchaguzi mkuu 2015.
No comments:
Post a Comment