Thursday 12 November 2015

SITTA, DK. NCHIMBI, PROFESA MAHALU, MARMO WAJITOSA KUWANIA USPIKA KUPITIA CCM





WAGOMBEA kumi wamechukua fomu ya kugombea kuteuliwa kwa nafasi ya uspika na unaibu spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Miongoni mwa waliochukua fomu ni Leonce Mulenda,Profesa Costa Ricky Mahalu, Samwel Sitta, Dk. Kalokola Muzzammil, George Nangale, Banda Sonoko,Gosbert Blandes, Simon Rubugu, Balozi Philip Marmo na Dk.Emmanuel Nchimbi.
Fomu hizo zilianza kutolewa jana, kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya Lumumba, jijini Dar es Saalam na Katibu wa Organezesheni, Dk.Muhammed Seif Khatib, kuanzia saa sita mchana.
Dk.Khatib alisema kwa wagombea ambao sio wabunge, mwisho wa kurejesha fomu hizo ni leo saa kumi jioni na kwa wale, ambao ni wabunge wateule, mwisho wa kuzirejesha ni keshokutwa.
“Baada ya kurejesha fomu, majina yao yatapelekwa  Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kuthibitisha kama wana sifa za kugombea nafasi hiyo,”alisema
Alisema hatua itakayofuata ni kuwajadili na kuwachuja kupitia Kamati Kuu ya CCM na Kamati ya Chama ndani ya bunge, ili kumchagua mmoja wao na kwamba vitu vitakavyozingatiwa ni masharti.
Alisema jumla ya wajumbe 246 watashiriki katika kupitisha jina hilo la mgombea.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu, spika wa zamani wa bunge, Samuel Sitta, alisema lengo kuu la kujitosa kwenye kinyanganyiro hicho ni kutokana na kuwa na sifa za kutosha na uzoefu mkubwa.
Alisema anataka kuendeleza mipango ya kimaendeleo ya bunge, ikiwemo kurejesha nguvu ya chombo hicho na hadhi yake.
“Katika bunge la tisa niliweka mipango hiyo, lakini kwa bahati mbaya ikashindwa kuendelezwa, lakini kwa sasa nina imani kuwa bunge hili litakuwa gumu kutokana na changamoto za kuwepo kwa suala la katiba, mambo ya siasa za ukanda na masuala ya kipato,”alisema
Kwa upande wake, Dk. Nchimbi alisema dhamira ya kujitokeza kuchukua fimu hiyo ni kutokana na changamoto za wakati huu, ambapo wabunge hawashiriki kikamilifu katika kuwaletea maendeleoa wananchi ipasavyo.
Dk.Nchimbi alisema kasi ya Rais Dk. John Magufuli inatakiwa kuendana sawa na viongozi wengine ili kutekeleza Ilani na ahadi za CCM, ambazo ni kuwaletea maendeleo Watanzania bila kujali itikadi za vyama.
“Ninachosema ni kwamba nimejitokeza kutokana na kujipima kuwa uwezo wangu ni mzuri, pia nina sifa za kushika nafasi hiyo kwa kasi kama ya Rais Magufuli ili kuwaletea maendeleo wananchi,”alisema
Wakati huo huo, CCM imetoa ratiba ya kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa uspika na unaibu spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo wana-CCM wasio wabunge wenye sifa walitakiwa kuchukua fomu jana.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM, ilisema fomu hizo zitatolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Oganaizesheni, Muhammed Seif Khatib na zilianza kutolewa jana, saa 6.00 mchana na mwisho wa kuzirejesha ni leo kabla ya saa 10 jioni.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, fomu zitatolewa kwa wana-CCM wenye sifa husika.

Katika taarifa hiyo, wana-CCM wasio wabunge wanaoomba ridhaa ya Chama kugombea uspika, wanatakiwa kuchukua fomu hizo katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam na kuzirejesha leo, kabla ya saa kumi jioni.

Aidha, taarifa hiyo ilisema wana-CCM, ambao ni wabunge wateule wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wanaoomba kuteuliwa kugombea uspika na unaibu spika wa bunge, walitakiwa kuchukua fomu kuanzia jana na kuzirejesha Novemba 14, mwaka huu, kabla ya saa kumi jioni, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment