Thursday 12 November 2015

VIONGOZI ACT-WAZALENDO WAMFAGILIA RAIS MAGUFULI




KASI ya utendaji ya Rais Dk. John Magufuli, imeendelea kuwakuna Watanzania ambapo, uongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, umeeleza kuvutiwa na kupongeza utendaji kazi wake.
Pia, umesema uamuzi wa Dk. Magufuli kuanza kudhibiti matumizi ya fedha za serikali kwa kuzuia safari za nje ya nchi kwa viongozi na watendaji wa wizara na taasisi, ni hatua ya kuungwa mkono.
Chama hichi kimesema uamuzi huo unadhihirisha dhamira ya kweli ya Dk. Magufuli kuwatumikia Watanzania na kuwabana watendaji kutimiza majukumu yao.
Hivi karibuni, Rais Magufuli alifuta safari za nje ya nchi kwa viongozi wa umma na kuagiza shughuli hizo ziwe zinafanywa na mabalozi.
Hata hivyo, Rais Magufuli alisema vibali vyote vya safari hizo vitakuwa vinatolewa na yeye mwenyewe pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kiongozi Mkuu wa ACT, Zitto Kabwe alisema anampongeza Dk. Magufuli kwa kudhibiti safari hizo.
Zitto alisema akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kamati yake iliagiza ufanyike ukaguzi maalumu wa safari za nje kwa viongozi na tayari ripoti imekamilika.
Zitto alimpongeza Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Anna Mghwira, kwa kushika nafasi ya tatu katika uchaguzi mkuu wa rais, ambapo katika wagombea wanane, mwanamke alikuwa peke yake.
Pia, aliwashukuru wananchi kwa kukiwezesha chama hicho kushika nafasi ya tatu katika kinyang’anyiro cha kumpata rais licha ya uchanga wake na kuviacha nyuma vyama vikongwe.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu ACT-Wazalendo, Samson Mwigamba amesema chama hicho hakitakuwa na mgombea wa uspika, badala yake wanajikita katika uchaguzi mdogo wa majimbo manane.
Mwigamba alisema hawatajihusisha katika mchakato wa kusimamisha mgombea wa uspika kwa sababu wamewekeza nguvu zaidi katika uchaguzi mdogo wa wabunge, ambao utafanyika katika majimbo manane, ambayo hayakupika kura Oktoba 25, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment