Thursday 12 November 2015

BAN KI-MOON AMPONGEZA RAIS MAGUFULI


KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon, amempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kushinda uchaguzi mkuu na kuchaguliwa kuwa rais mpya wa Tanzania.

Katika barua yake ya salamu za pongezi kwa Dk. Magufuli, Ban, alisema anaamini chini ya uongozi wa Dk. Magufuli, Tanzania itajikita katika kuondoa umaskini, kuimarisha utawala bora na kuendeleza juhudi zake kwenye kupigania amani na utulivu katika eneo lote la Afrika Mashariki na Maziwa Makuu.

“Uchaguzi wa mwaka 2015 ni uthibitisho wa wazi na dhamira ya muda mrefu ya Watanzania kuendeleza demokrasia, amani na utulivu. Nina imani kuwa mambo machache yaliyosalia kutokana na uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu, yatashughulikiwa kulingana na taratibu za kisheria kwa amani na uwazi.

“Nakuhakishia kuwa UN itaendelea kukuunga mkono pamoja na serikali yako katika juhudi hizi za maendeleo,”alisema.

Aidha, alisema anaipongeza Tanzania kwa kuendelea kuwa mshirika imara na wa kutumainiwa katika Umoja wa Mataifa kwa kipindi chote cha uanachama wake tangu ilipojiunga hadi sasa.

Katibu Mkuu huyo alisema anathamini ushirikiano uliopo kati ya UN na Tanzania katika kuendeleza malengo ya umoja huo na kuitakia mafanikio kwenye kutekeleza shughuli zake.

No comments:

Post a Comment