Tuesday, 4 July 2017
SISAFIRI NJE NG'O-JPM
RAIS Dk. John Magufuli, amesema hatasafiri kwenda nje ya nchi ili kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa wananchi kwani kuondoka kwake kutawapa nafasi mafisadi kuharibu nchi.
Amesema hadi sasa amepata mialiko 60, kutoka nchi mbalimbali, lakini hatakwenda, bali ataendelea kutuma wawakilishi wanaofanya kazi nzuri kwa niaba yake.
Rais Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana, mjini Sengerema, alipokuwa akizindua mradi wa maji wa Nyamazugo, mkoani Mwanza.
Alisema hawezi kusafiri kwa sababu baadhi ya Watanzania ni wajanja, hivyo anaweza kwenda huko wakafanya mambo yao.
"Ndiyo maana naomba mniombee ili niyashughulikie haya, niyanyooshe. Nisipoyashughulikia haya, nitamaliza kipindi changu na yatabaki hivyo hivyo.
"Ndiyo maana sitembei sana, nimeshapata mialiko karibia 60, iendi, nikienda huko watafanya ya ajabu, ngoja ni-deal nao kwanza huku. Watanzania wajanja, lazima nihakikishe nimesafisha kwanza," alisema.
Rais Dk. Magufuli alisema alitakiwa kuwepo nchini Ethiopia kwenye Mkutano wa Umoja wa Afrika (AU), lakini aliona amtume Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ili amwakilishe na yeye aendelee na majukumu mengine.
"Sisafiri sasa hivi, lazima niwanyooshe kwanza. Hizi safari zipo. Nikistaafu, nitakwenda tu Ulaya, lakini kwa sasa ngoja kwanza," alisisitiza.
Dk. Magufuli alisema aliahidi kuwa atakapoingia madarakani, atashughulika na suala la rushwa na ufisadi, ambalo limekuwa ni saratani kwa Watanzania.
"Tumeanza kuchukua hatua, tumetengeneza sheria ya kupambana nao. Tunataka Tanzania inyooke ili siku nikitoka niache imenyooka, yule atakayekuja aje atawale vizuri kwa sababu lazima kuwepo na mtangulizi," alisema Rais Magufuli.
Aliongeza: "Tumechezewa sana, kwenye madini huku tumeibiwa sana. Zaidi ya shilingi trilioni 388, zimeondoka, bajeti yetu ni shilingi trilioni 30, kwa hiyo zingetosha kwa miaka 12. Dhahabu zinasombwa utafikiri sisi hatuna ubongo. Na waliokuwa wakihusika ni viongozi wa serikali."
"Fedha zilizokuwa zinachukuliwa hapa inawezekana zinaendesha hata nchi nyingine huko halafu sisi wanatuletea mitumba tunavaa. Ndugu zangu mimi ndiyo rais wa nchi hii na mimi ndiyo najua siri za nchi hii," alisema.
Aidha, alisema anawaambia ukweli Watanzania kwa sababu hakuna mtu, ambaye angejitolea kueleza ukweli kama anavyofanya yeye.
Rais Dk. Magufuli alisema hakuwa kichaa kuzuia makontena yote yale, tena ya vigogo, lakini alifanya hivyo kwa ajili ya Watanzania, ambao ni masikini kwa sababu asingefanya hivyo, hakuna mwingine ambaye angefanya.
"Mnaponiona nasimama hapa tena hadharani bila kuogopa rangi ya mtu, ninafanya hivi kwa niaba yenu. Naomba niwaambie ndugu zangu, tutashinda kwa sababu Mungu yupo pamoja na sisi," alisema.
NGO ZIFUNGUE SHULE ZAO
Akizungumzia kuhusu wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shuleni, Rais Dk. Magufuli alisema kuna watu wanazungumza kuwa wanafunzi wanaopata mimba waendelee kusoma, jambo ambalo haliwezekani.
"Nihangaike kukusanya kodi za Watanzania, nikakusomeshe bure halafu na wewe ukapate mimba bure. Haiwezekani, wewe unasoma bure, kafuate kile ambacho kimekupeleka kusoma.
"Tunataka Watanzania wapate elimu ya kweli, tukiruhusu suala hili tutaingia kwenye mtego wa ajabu, kwa sababu mtu atafika darasa la nne atapata mimba, atakwenda kuzaa, atarudi tena atapata tena,"alisema.
Rais Dk. Magufuli alisema mtoto huyo akishapata mimba, mchezo huo atakuwa ameuzoea, hivyo akirudi shuleni atakwenda kuwa mwalimu wa wanafunzi wengine wasiojua.
"Ni lazima sisi kama wazazi tusimame kama wazazi, tuache mambo ya kukopi. Siyo kwamba ninawachukia wenye mimba, akifanikiwa amepata mimba aende akatafute shule nyingine zinazotaka wenye mimba," alisema.
Kutokana na hali hiyo, aliziomba NGO zinazowatetea wanafunzi hao, kufungua shule za wenye mimba kwa sababu zinawapenda watu hao.
"Wao wanapewa fedha za kufanya makongamano na kuelimisha jamii, lakini sasa wanazitumia kwa ajili ya kuwatetea wenye mimba," alisema.
Pia, aliwaonya wakuu wa shule, ambao watawaruhusu wanafunzi waliopata mimba kurudi shuleni kuwa watafukuzwa kazi.
Akizungumza na wananchi wa Sengerema na Buchosa, Rais Magufuli alisema wameamua katika maeneo ya vijijini, wananchi waweze kupata maji kwa asilimia 85 na mijini 95.
Kutokana na hali hiyo, aliwapongeza watendaji wa Wizara ya Maji wakiongozwa na Waziri wao, Mhandisi Gerson Lwenge kwa kazi nzuri waliyoifanya hasa katika suala zima la maji.
"Waziri leo nakupongeza sana na hasa uliponiambia kuwa ule mradi wa Ng'apa (Lindi), ambao kwa kweli nilipanga kukufukuza kama mradi ule usingekamilika.
"Kwa hiyo sasa hivi naona umefanikiwa, hongera sana, ukae kwa raha Mhandisi Lwenge, kama kweli yale maji yameanza kutoka kule Lindi, wewe kwa kweli ni mwanaume safi," alisema.
Pia, alimpongeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Kitila Mkumbo kwa utendaji wake wa kazi.
"Profesa Kitila yeye alikuwa ACT-Wazalendo, lakini ni mchapakazi. Vilevile aliahidi kutekeleza Ilani ya CCM, nikampa ukatibu mkuu. Hii ni katika kudhihirisha maendeleo hayana chama, anafuata maagizo ya CCM bila kupindisha," alisema.
Alisema Watanzania wamechoka kusikia mambo ya vyama na wanataka maendeleo kwa sababu hawawezi kula chama.
Kuhusu mradi huo wa maji, alisema kwenye mikoa mingi hivi sasa kuna miradi mikubwa ya maji, ambayo inatekelezwa katika hatua mbalimbali.
"Katika mkoa huu wa Mwanza, mbali na mradi huu wa Sengerema, tumekamilisha mradi wa maji wa Nansio, tunaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji safi katika jiji la Mwanza, hasa katika miji ya Magu na Misungwi," alisema Rais Dk. Magufuli.
Alisema miradi hiyo itatekelezwa na serikali kwa kushirikiana na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya na Shirika la Maendeleo la Ufaransa, kwa gharama ya sh. bilioni 69.3, ambapo unatarajiwa kukamilika Agosti, 2019.
Mbali na mradi wa mkoa wa Mwanza, pia alisema wapo kwenye hatua nyingine ya kuhakikisha maji safi yanapatikana mkoani Geita.
"Mradi huu una thamani ya shilingi bilioni 250, unatekelezwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Hifadhi ya Mazingira Duniani," alisema.
Alisema wananchi wengi wanaoishi kandokando ya Ziwa Victoria, wamezungukwa na maji, lakini wana tatizo kubwa la ukosefu wa maji.
UVUVI HARAMU
Akizungumzia uvuvi haramu, alisema wananchi wanaoishi kandokando ya ziwa hilo, wanapenda kutumia uvuvi haramu kwa ajili ya kuvua samaki.
"Hata hapa wanafanya uvuvi haramu na mimi nafahamu na kuna baadhi ya viongozi wanashirikiana nao, nawafahamu watumia kokoro na madawa.
"Sasa mkiyaweka yale madawa ziwani, yanakuja hadi sehemu tunakovutia maji, yataingia kwenye bomba, yatavutwa, yataingia humo na hivyo mtawapa watu sumu, watu zaidi ya 138,000. Jiulize wewe mvuvi umefanya mauaji ya namna gani? Wewe ulitaka upate kamongo, lakini umekwenda kuleta madhara kwa Watanzani wengi," alisema.
Aliongeza: "Hata wasipokufa, ndo utakuta watu wana magonjwa ya saratani, mimba kuharibika na wanaume nao nguvu zinapungua kwa sababu ya mtu mmoja tu."
Rais Magufuli aliwataka wavuvi kuacha uvivu haramu kwa sababu ni hasara kwa maisha ya Watanzania.
Pia, aliagiza vyombo vya dola, watendaji wa kata na viongozi wote kulisimamia suala hilo kwa sababu katika Hospitali ya Ocean Road, wagonjwa wengi wa saratani wanatoka Kanda ya Ziwa.
"Ni lazima tujiulize kwa nini kanda ya ziwa? Wagonjwa wengi wa saratani wanatoka hapa, hii ni sababu ya wavuvi wenye tamaa kuamua kutumia madawa na kusababisha madhara makubwa," alisema.
Vilevile, aliagiza OCD, Wakuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kuwa wakali katika suala hilo ili kuepusha madhara, ikiwa ni pamoja na kuokoa maisha ya Watanzania.
MIRADI YA UMEME
Alisema serikali imeamua kuanzisha miradi mikubwa ya umeme kwa ajili ya kuendesha viwanda vitakavyojengwa nchini.
"Naamini tutakapokuwa na umeme mwingi, viwanda vyetu vitakuwa vinapata umeme wa kutosha," alisema.
Awali, Waziri Lwenge aliwaomba wananchi watakaonufaika na miradi hiyo, kulipia bili zao za maji kwa ukamilifu, ikiwa ni pamoja na kulinda miundombinu yake ili kuwa endelevu.
Pia, alitoa wito wa wananchi kuepuka uharibifu wa mazingira ili kuweza kulitunza Ziwa Victoria.
"Natoa wito kwa wananchi kutunza vyanzo vya maji na kuacha kulima kwenye vyanzo hivyo," alisema.
Kuhusu mradi wa maji wa Lindi, alisema umeanza kusukuma maji kuingia kwenye tanki kubwa na wananchi wataanza kupata huduma hiyo muda wowote kuanzia sasa.
Katibu Mkuu Profesa Mkumbo alisema ukamilikaji wa mradi huo utawezesha upatikanaji wa maji kwa asilimia 100.
Naye Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba alisema mradi huo ni mkubwa na pia utavinufaisha baadhi ya vijiji vilivyoko kwenye jimbo la lake la Buchosa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja alisema kwa niaba ya wananchi wake kuwa, wanaahidi kutunza miundombinu ya mradi huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment