Tuesday, 4 July 2017

WABUNGE SABA WA CHADEMA WAHOJIWA NA POLISI

SAKATA la kutishiwa kupigwa kwa mbunge wa Viti Maalum (CCM), Juliana Shonza, limechukuwa sura mpya baada ya wanaodaiwa kufanya tukio hilo kuhojiwa na jeshi la polisi mkoani hapa.

Akizungumza na Uhuru, kwa njia ya simu, jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Ernest Kimola, alithibitisha kuhojiwa kwa wabunge saba wa CHADEMA.

“Ni kweli jana (juzi), tuliwahoji wabunge saba wa CHADEMA, ambao wanadaiwa kumzonga zonga na kutaka kumpiga Juliana. Hivi sasa tunakamilisha taratibu za upelelezi ili tuweze kuchukua hatua stahiki,” alisema Kimola bila ya kuyataja majina ya wabunge hao kwa madai alikuwa nje ya ofisi.

Hata hivyo, juzi jioni, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema wabunge wanaotuhumiwa kumzonga zonga na kutaka kumpiga Juliana ni Said Kubena (Ubungo), Joseph Thelathini (Rombo), Devota Minja (Viti Maalum), Susan Kiwanga (Mlimba), Cecil Mwambe (Ndanda), Frank Mwakajoka (Tunduma), Cecilia Pareso (Viti Maalum) na Paulina Gekul (Babati Mjini).

Alisema tuhuma zinazowakabili wabunge hao ni kosa la jinai na pia watapelekwa kwenye kamati ya haki, maadili na madaraka ya bunge.

Ndugai alisema suala hilo kwa jinsi alivyolipokea ni la kijinai na kwamba, mara zote wanawaelekeza wabunge wanapokuwa ndani ya bunge kuwa hawana kinga dhidi ya makosa ya jinai.

Ndugai alisema aliombwa na Juliana ili ampe kibali cha kulifikisha suala hilo kwenye vyombo vya dola ili lifanyiwe kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za kijinai.

Alisema suala hilo kwa sababu ni la kimaadili na kwa mujibu wa sheria na kanuni, masuala yote ya kimaadili yanafanyiwa kazi na kamati ya haki, maadili na madaraka ya bunge.

“Hivyo basi, kwa mujibu wa kanuni ya 4 ya nyongeza ya 8 ya kanuni za bunge toleo la Januari 2016, nimelipeleka suala hili mbele ya kamati ya maadili ili ilifanyie uchunguzi na nini hasa kilitokea, nani walihusika na kisha kutoa maoni na mapendekezo kuhusu hatua za kuchukua,” alisema.

Aliwaomba wabunge kujiepusha na makosa ya kijinai na kwamba, mambo ya kijinai yanafanyiwa kazi na vyombo vya dola, ambapo pia aliwahimiza wabunge suala la maadili na kuishi kiutu na ushirikiano.

Alisema vurugu hizo zilitokea baada ya shughuli za bunge kusitishwa kwa mapumziko ya mchana na tukio hilo lilitokea katika lango la kuingilia jengo la utawala ofisi ya bunge.

Ndugai alisema katika tukio hilo, Juliana alikutana na baadhi ya wabunge wa kambi ya upinzani, ambao walirushiana maneno na kumzonga zonga kwa nia ya kutaka kumpiga.

Alisema wabunge hao walitaka kumpiga Juliana, kutokana na utendaji wake kazi bungeni, hususan hoja yake aliyoitoa Juni 5, mwaka huu, ya kubadilisha pendekezo la adhabu lililotolewa na kamati ya haki, maadili, madakara ya bunge kwa Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda) wa CHADEMA.

Alisema hoja ya Juliana ilisababisha bunge kuazimia kuongeza adhabu kwa wabunge hao.

Spika alisema sheria na kanuni za bunge zinatoa makatazo na zinaainisha vitendo mbalimbali, ambavyo ni makosa na havitakiwi kabisa kufanyika maeneo ya bunge.

No comments:

Post a Comment