Tuesday, 4 July 2017

DC HAPI AAGIZA MBUNGE HALIMA MDEE AKAMATWE


MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi, ameagiza polisi wilayani humo kumkamata mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), kwa kosa la kutoa kauli za matusi, dhihaka na uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.

Pia, amesema wilaya yake sio ya kuchezewa na wanasiasa kwa kutoa maneno ya kejeli dhidi ya Rais na viongozi wengine wa serikali.

Hapi amesema yeye kama mwenyekiti wa ulinzi na usalama katika wilaya hiyo, anataka Halima akamatwe na kuhojiwa kwa saa  48 na afikishwe kwenye vyombo vya sheria .

“Namtaka Halima akae saa 48 korokoroni ili aweze kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi, aeleze hayo aliyoyasema kama yapo sawa kisheria,” aliagiza Hapi alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, jana.

Hapi alisema kitendo cha Halima kumwambia Rais Magufuli kuwa ana tabia za hovyo, ni kosa kubwa kisheria kwa kumtolea maneno hayo kiongozi wa nchi, ambaye alichaguliwa kwa kura za wananchi.

Alisema Ibara ya 33 ya kanuni ya sheria ya nchi, haimruhusu mtu kumtolea maneno ya dhihaka kiongozi wa nchi.

“Halima amekosea sana, amepindisha kanuni za nchi kwa kutoa maneno ya uchochezi kwa kusema 'ipo siku rais ataagiza wanawake na wanaume watembee vifua wazi,'" alisema.

Hapi alisema kauli hiyo ni ya uchochezi kwa Watanzania na kwamba, kiongozi kama mbunge hapaswi kuchochea vitu, ambavyo hapo baadaye vinaweza kuleta madhara kwa Taifa.

Hapi alisema mbunge huyo anatakiwa kutafutwa na kukamatwa kisha kuwekwa rumande kwa saa 48, huku akihojiwa sababu za kutaka kuvuruga usalama.

Kiongozi huyo alisema ameamua kutoa agizo hilo kufuatia hatua ya mbunge huyo wa Kawe kwa tiketi ya CHADEMA, kufanya mkutano wa wanahabari makao makuu ya chama hicho juzi, jijini Dar es Salaam na kutoa maneno yasiyo ya kiungwana.

Aidha, alisema kukamatwa kwa Halima litakuwa fundisho kwa watu wenye tabia kama yake ya kudharau viongozi wa nchi, akiwemo rais.

No comments:

Post a Comment