Thursday 5 November 2015

MZEE MKAPA YU MZIMA WA AFYA





SERIKALI imekanusha uvumi ulioenea kuhusu kifo cha Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa na kusema yupo hai, buheri wa afya na yanayosemwa ni uzushi mtupu.

Aidha, imesema inaendelea kufuatilia chanzo cha uvumi huo na kwamba itachukua hatua kali dhidi ya atakayebainika kuhusika.

Msenaji Mkuu wa Serikali, Assah Mwambene, alisema hayo jana, jijini Dar es Salaam, na kuongeza kuwa Mkapa ni mzima wa afya na anaendelea na shughuli zake kama kawaida.

“Rais Mstaafu Mkapa, ni mzima, haumwi hata mafua wala malaria, tunalaani kitendo hiki cha uzushi na tunatumia nguvu kubwa kuhakikisha hatua zinachukuliwa kwa aliyeanzisha habari hii,” alisema.

Alisema si jambo zuri kumzushia kiongozi yeyote habari mbaya kama hizo na kuita kuwa huo ni uchuro, kwa kuwa zilipoanza kusambaa Rais huyo Mstaafu alikuwa visiwani Zanzibar kikazi.

Alisisitiza kuwa serikali inawataka wananchi kuacha mara moja kusambaza ujumbe huo unaoenea kwa kasi, ambao si mzuri na unalishushia hadhi taifa. 

Mwambene alisema, Mkapa amekuwa kiungo muhimu kuhusu amani na mustakabali wa taifa hususani kipindi hiki tangu zilipoanza kampeni za uchaguzi mkuu.

Kuhusu watu wanaoanzisha habari za uzushi kupitia mitandao ya kijamii, alisema serikali imekusudia kuongeza kasi ya kuwakamata watu hao na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

No comments:

Post a Comment