GIZA nene limezidi kugubika Mradi wa Mabasi Yaendayo
Haraka Dar es Salaam (DART), ambapo mpaka sasa dalili za kuanza kazi hazipo
licha ya wananchi kusubiri kwa hamu kubwa.
Aidha, agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutaka
mradi huo kuanza kutoa huduma ifikapo Januari 10, mwaka huu, limeshindwa
kutekelezwa huku ukimya ukizidi kutawala.
Utata zaidi umeibuka baada ya mabasi 140 ya mradi huo,
kuwekwa chini ya Kamishna wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),
kutokana na kudaiwa ushuru.
Mabasi hayo ambayo yamehifadhiwa kwenye Bandari Kavu
chini ya TRA, yamezuiwa hadi hapo kodi inayodaiwa itakapolipwa yote ndipo
yatolewe na kukamilishwa taratibu za usajili.
Wakati TRA ikiyazuia mabasi hayo, kampuni inayoendesha
mradi huo, UDA-RT bado inaendelea kuvutana na mamlaka za serikali kuhusu
viwango vya nauli vitakavyotumika kwenye mabasi hayo.
Awali, mapendekezo ya UDA-RT kuhusiana na nauli za
mabasi ya mradi huo, zilipingwa vikali na wadau kutokana na kuwa kubwa mara
mbili ya zinazotozwa sasa.
Kufuatia mvutano huo, kampuni hiyo imedai kamwe haiwezi
kulipia kodi mabasi hayo hadi hapo mzozo wa nauli utakapopatiwa ufumbuzi.
Januari 6, mwaka huu, Waziri Mkuu Majaliwa, alisema
viwango vya nauli vilivyopendekezwa na UDA-RT ni vikubwa na serikali
haitakubaliana navyo.
Pia, alionya kuwa iwapo mwafaka wa viwango hivyo
hautapatikana, serikali haitosita kuchukua mradi huo na kuuendesha ili wananchi
wapate huduma bora na nafuu.
Viwango vya nauli vilivyopendekezwa vilikuwa kuanzia sh.
700 kutoka Mbezi hadi Kimara, sh. 1,200 kutoka Mbezi hadi Kivukoni huku nauli
ya kutoka Mbezi-Kimara-Ubungo hadi Mwenge ikiwa ni sh. 1,400. Katika viwango
hivyo, mwanafunzi atatakiwa kulipa nusu ya nauli ya mtu mzima.
Viwango vinavyolipwa kwa sasa na abiria kwenye daladala
ni sh. 400 kutoka Mbezi hadi Kimara na sh. 500 kutoka Kimara hadi Kivukoni huku
mwanafunzi akilipa sh. 200.
Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipa Kodi wa TRA,
Richard Kayombo, alipoulizwa kuhusiana na kuzuiwa kwa mabasi hayo, alisema hatua
hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa taratibu za forodha.
Alisema mabasi hayo yaliyoko kwenye mradi huo, yataendelea
kuwa chini ya usimamizi huo hadi hapo taratibu za ulipaji kodi pamoja na usajili
zitakapokamilika.
“Mabasi hayo yapo chini ya Kamishna wa Forodha hadi
utaratibu wa malipo ya kodi na usajili utakapokamilika,” alisema Kayombo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Simon Group,
Robert Kisena, ambayo ni mmiliki mwenza wa UDA na mbia kwenye kampuni ya UDA-RT
iliyopewa mradi huo, alikiri TRA kuyazuia mabasi hayo.
Hata hivyo, alisema hawawezi kuyalipia mabasi hayo hadi
hapo utata kuhusiana na viwango vya nauli kati ya UDA-RT na serikali utakapopatiwa
ufumbuzi.
“Ni kweli mabasi yamezuiwa, lakini hatuwezi kuyalipia kodi
wakati bado hatujafikia makubaliano kwenye viwango vya nauli…hatuna uhakika
iwapo ufumbuzi wa suala hili utapatikana kwa haraka,” alisema Kisena.
Kufuatia kuzuiwa kwa mabasi hayo na utata kuhusiana na
umiliki sahihi wa UDA, Ofisa Uhusiano wa Hazina, Gerald Chami, alisema serikali
kupitia Msajili wa Hazina inamiliki asilimia 49 ya hisa za UDA.
Hata hivyo, alisema UDA ni miongoni mwa mashirika ambayo
serikali ina hisa zake, yanayofanyiwa uchunguzi kuhusiana na taarifa na
mwenendo wake kiutendaji.
Alisema hatua hiyo imetokana na baadhi kusuasua kwenye
utendaji huku mengine yakishindwa kutoa gawio kwa serikali kikamilifu.
“Kama unavyofahamu kuhusu tangazo lililotolewa na
serikali kuhusu mashirika yaliyobinafsishwa kutakiwa kutoa taarifa za
uendeshaji wake, hivyo baada ya kupitia, tutatoa tamko,” alisema Chami.
Alisema bado mwenendo wa shirika hilo katika utoaji
gawio kwa serikali sio wa ufanisi.
AGIZO
LA WAZIRI MKUU
Novemba 25, mwaka jana, Waziri Mkuu Majaliwa aliwaagiza
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mtendaji Mkuu wa DART, Wakala wa Barabara
Tanzania (TANROADS) na Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, wapitie
masuala yote ya kisheria yanayohusu mradi na kuhakikisha miundombinu inakamilika ili uanze kutoa
huduma mapema.
Lakini pia, Desemba 19, mwaka jana, akitembelea
miundombinu ya mradi huo, Waziri Mkuu Majaliwa aliagiza mabasi yaanze kutoa
huduma kwa wananchi ifikapo Januari 10, mwaka huu. Leo ni Januari 14, zikiwa ni
siku nne zaidi ya zile zilizoagizwa.
Waziri Mkuu Mjaliwa, pia aliagiza kukamilishwa kwa
ujenzi wa vituo vikuu vya kushusha na kupakia abiria vya Kivukoni, Morocco,
Jangwani na Kimara sambamba na kupitiwa kwa mikataba ya ubia kati ya DART, UDA
na Chama cha Wamiliki wa Daladala (DARCOBOA).
Alisema serikali haitaki kusikia kuwepo kwa malalamiko
miongoni mwa wadau wa DART, hivyo lazima kila upande unaohusika unufaike.
Licha ya maagizo hayo kutolewa mwaka jana, lakini bado
baadhi ya vituo vya mradi huo havina dalili za kuwa tayari kwa kutoa huduma.
Hata hivyo, imebainika kuwa baada ya kupitiwa kwa
mikataba na nyaraka mbalimbali imebainika kuwa, hakuna mpango wa biashara
ulioandaliwa na kampuni ya UDA-RT iliyopewa jukumu la kutoa huduma za mpito za
usafiri huo.
Ilibainika kuwa gharama za uwekezaji ikiwemo ununuzi wa
magari, vifaa vya kutozea nauli na gharama nyingine haziko bayana.
Baada ya kubainika kwa utata huo, kupitia mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika Januari 6, mwaka huu, Waziri Mkuu Majaliwa alisema
kukosekana gharama halisi za uwekezaji ni dhahiri kuwa viwango vya nauli
vinavyopendekezwa UDA-RT, havina uhalisia.
“Serikali haikubaliani na mapendekezo hayo ya nauli kwa
sababu gharama za uwekezaji za mwekezaji huyo hazifahamiki na hakuna mpango wa
biashara unaoeleza mtiririko wa biashara ya mabasi hayo,” alisisitiza.
Alisema kwa tafsiri ya viwango hivyo vya nauli, kwa
mtumishi mwenye kima cha chini cha mshahara wa 260,000 kwa mwezi, akiwa na
familia atatumia zaidi ya robo tatu ya mshahara wake kwa kulipa nauli.
Kutokana na utata kugubika mradi huo, tayari serikali
imemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa DART, Asteria Mlambo, kwa kushindwa kuzingatia
Sheria ya Manunuzi ya Umma wakati wa kumpata mtoa huduma katika kipindi cha
mpito.
No comments:
Post a Comment