Tuesday, 4 July 2017

SARE ZA JWTZ ZAMPONZA MANJI, AKUTWA NA MIHURI 39 YA TAASISI MBALIMBALI


POLISI mkoani Dar es Salaam, inamshikilia mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji, kwa tuhuma za kukutwa na nyara za serikali, mali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Kaimu Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, amesema mfanyabishara huyo alikutwa na majora 43, za sare za JWTZ na mihuri 39 ya taasisi mbalimbali.

Mkondya alisema baada ya kukamata vitu hivyo, Julai Mosi, mwaka huu,  walimkamata Manji akiwa kwenye eneo la ofisi zake za Quality Center.

Mkondya alisema katika mihuri 39, waliyomkamata nayo, minne ni mali ya vikosi vya JWTZ.

Alifafanua kuwa kwa sasa wanamshikilia mfanyabiashara huyo kwa ajili ya kumhoji sare  hizo alizitoa wapi na nini madhumuni ya kuziingiza nchini.

“Manji tupo naye kwa ajili ya kumhoji juu ya sare  za JWTZ na mihuri kaitoa wapi na nini dhumuni lake la kuwa na vitu visivyo vyake,”alisema.

Kaimu Kamishna huyo alisema wanatarajia kumfikisha Manji mahakamani wakati wowote upelelezi utakapokamilika.

Wakati huo huo, Furaha Omary, anaripoti kuwa, Manji na wenzake wawili wamewasilisha maombi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, wakiiomba iwaachie kutokana na kukamatwa na kushikiliwa isivyo halali.

Aidha, wanaiomba mahakama hiyo, itoe amri  kwa walalamikiwa, akiwemo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ili waweze kufikishwa mahakamani na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Manji, Deogratius Kisinda na Thobias Fwere, waliwasilisha maombi hayo kwa hati ya dharura huku walalamikiwa wakiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO).

Mfanyabiashara huyo na wenzake wamewasilisha maombi hayo yakiwa yameambatanishwa na hati ya kiapo cha Wakili Hudson Ndusyepo kwa ajili ya kuyaunga mkono.

Kupitia hati ya kiapo, Wakili Ndusyepo ameeleza kuwa, walalamikiwa walikamatwa na kushikiliwa na ZCO kwa nyakati tofauti, ambapo Kisinda alikamatwa Juni 30, mwaka huu, saa 10, Manji na Fwere walikamatwa Julai mosi, mwaka huu, saa tano katika jengo la Quality Centre, lililoko pembezoni mwa barabara ya Pugu.

“Tangu siku hiyo wameendelea kushikiliwa Kituo cha Polisi cha Kati,” alidai Ndusyepo na kuongeza kuwa, alifahamishwa na ZCO kwamba, Manji na wenzake walikamatwa na kushikiliwa kwa tuhuma za kutenda kosa linalohusiana na sare, ambazo zilikamatwa kwenye stoo ya Quality Motors Limited.

“Kukamatwa kwa walalamikaji sio halali kwa sababu kosa linalodaiwa, ambalo lilisababisha kukamatwa kwao na kushikiliwa, linahusiana na masuala ya Kampuni ya Quality Motors, ambayo inaongozwa na wakurugenzi wake na sio walalamikaji,” alieleza Ndusyepo kupitia hati yake hiyo ya kiapo.

Wakili huyo alidai baada ya kukamatwa walalamikaji, akiwa wakili wao, aliwaombea dhamana, lakini maombi hayo yalikataliwa kwa sababu ambazo hazijajulikana.

“Kama wakili wa waombaji, nilikuwa nafuatilia dhamana zao tangu walipokamatwa na kushikiliwa hadi hivi sasa, zaidi ya saa 48 zimepita na ZCO amekataa kuwafikiria kuwapa dhamana kwa sababu anazojua mwenyewe,” alidai.

Wakili huyo alieleza kuwa, anafahamu na kwa uelewa wake wa sheria na uzoefu akiwa wakili, vitendo vya walalamikiwa kuendelea kuwashikilia walalamikaji zaidi ya saa 48 na kukataa kuwapa dhamana ni kinyume cha sheria na sio sahihi.

Ndusyepo alidai kutokana na ukiukwaji huo wa sheria unaoendelea, kama mahakama haitakubali maombi  yao, walalamikaji wataendelea kuumia kwa kuingiliwa uhuru wao bila sababu za msingi na kwa msingi huo vitendo vya walalamikiwa havikubaliki.

“Hivyo itakuwa haki kwa mahakama kuingilia kati na kutoa maelekezo kama inavyostahili,” aliomba Ndusyepo.

Maombi hayo yamepangwa mbele ya Jaji Lugano Mwandambo, lakini bado hayajapangiwa tarehe ya kutajwa ama kuanza kusikilizwa.

No comments:

Post a Comment