Monday, 4 January 2016
FAMILIA YA MSAIDIZI WA IGP YAFA AJALINI
NA THEODOS MGOMBA, DODOMA
WATU wanane wa familia ya Msaidizi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Gerald Rioba, wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji katika eneo la Kibaigwa.
Wakati familia hiyo ikikutwa na majanga, watu wengine wanne wamefariki dunia na 35 kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha basi la Kampuni ya Luwinzo, lifanyalo safari zake kati ya Njombe - Dar es Salaam, baada ya kulivaa lori kwa nyuma lililokuwa limebeba makaa ya mawe.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema jana kuwa, tukio lililohusisha ajali ya Rioba, lilitokea juzi saa tatu usiku.
Alisema mwili wa msaidizi huyo wa IGP ulifanikiwa kupatikana jana, saa nne asubuhi, baada ya utafutwaji uliofanywa na Jeshi la Polisi na wananchi.
Misime alisema walipokea taarifa ya kuwepo kwa maji mengi yaliyosababisha magari kushindwa kupita katika eneo la Bwawani.
Misime alisema walipofika eneo la tukio, watu waliwaeleza kuwa wameona matairi ya gari yakiwa juu, umbali mdogo kutoka barabara Kuu.
Alisema baada ya kuinua gari hilo, ambalo lilikuwa limeharibika, walifanikiwa kukuta mwili wa Faida John, ambaye inasadikiwa ni mke wa Rioba.
Alisema baada ya kuendelea na utafutaji, walifanikiwa kupata miili mingine ya askari mwenye namba F 32 Koplo Ramadhani, mwili wa mtoto Gabriel Rioba (4) na Godwin Rioba, ambaye umri wake bado haujajulikana.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, jana asubuhi waliendelea kutafuta miili mingine na ndipo walipofanikiwa kupata mwili wa mtu aliyejulikana kwa jina la Ludege, ambaye ni Ofisa Mifugo wa Kata ya Panda Mbili na Sara Mbuga, ambaye ni mtumishi wa ndani.
Alisema mwili mwingine uliopatikana haujajulikana ni wa nani na uchunguzi zaidi unaendelea kuhusiana na tukio hilo.
Alisema marehemu hao walikuwa wakitokea Geita kwenda Jijini DareSalaam, wakiwa katika gari lenye namba za usajili T 516 DEP.
Katika hatua nyingine, Anita Boma, anaripoti kutoka Iringa kuwa watu wanne wamefariki dunia na wengine 35 wamejeruhiwa katika ajali iliyolihusisha basi la Kampuni ya Luwinzo, lifanyalo safari zake kati Njombe - Dar es Salaam.
Katika ajali hiyo, basi la Luwinzo lilivaa kwa nyuma lori lililokuwa limebeba makaa ya mawe.
Ajali hiyo ilitokea jana, saa moja asubuhi katika eneo la Kinegembasi, Kata Mbalamaziwa, wilayani Mufindi, katika barabara kuu ya Iringa –Mbeya, ambapo basi hilo lilikuwa likitokea Njombe kwenda Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, ACP Peter Kakamba, alisema ilihusisha basi hilo lenye namba za usajili T 782 AZR la Kampuni ya Luwinzo na lori lenye namba za usajili T 718 CRV na tela lenye namba za usajili T 529 ART, ambalo lilikuwa limebeba makaa ya mawe yakisafirishwa kutoka Songea kwenda Tanga .
Alisema basi hilo lilikuwa katika mwendo kasi, ambapo lilijaribu kulipita gari lingine bila ya kuangalia mbele kama kuna gari na kuamua kurudi ghafla, hivyo kuliingia kwa nyuma lori hilo na kusababisha vifo vya watu wanne ambao wote ni wanaume.
Kamanda Kakamba alisema watu wawili walifariki dunia papo hapo, ambao ni Rashid Kibalabala (47), ambaye alikuwa kondakta wa basi hilo na Salim Changwila (28), ambaye alikuwa mkaguzi wa basi hilo, huku mmoja alifariki akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Mafinga na mwingine alifariki akiwa anapatiwa matibabu.
Akizungumzia majeruhi, Kakamba alisema walikuwa 35, ambapo wawili wamelazwa katika Hospitali ya Makambako na wengine 33 walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mufindi.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni kosa la dereva wa basi aliyekuwa akijaribu kupita gari lingine bila ya kuangalia mbele kama kuna gari linakuja huku akiwa katika mwendo kasi.
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mufindi, Innocent Mhagama, alithibitisha kupokea majeruhi hao na maiti mmoja huku mtu mwingine akipoteza maisha akipatiwa matibabu, ambaye alitambulika kwa jina la Atupele Lusekelo Swebe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment