Monday, 4 January 2016
SERIKALI YANUNUA MASHINE MPYA YA CT-SCAN MUHIMBILI
Na Magreth Kinabo –MAELEZO
SERIKALI imenunua mashine mpya ya CT-Scan yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 1.7, ambayo ina uwezo wa hali ya juu kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Ununuzi wa mashine hiyo ulifanyika kufuatia agizo la Rais Dk. John Magufuli, alilolitoa alipoifanya ziara hivi karibuni hospitalini hapo, ambapo aliutaka uongozi wa hospitali hiyo kuboresha huduma zake na kuhakikisha vifaa tiba na dawa vinapatikana ili Watanzania wapate huduma bora za afya.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla, alisema hayo jana mjini Dar es Salaam, alipotembelea hospitali hiyo, ambapo alitembea Idara ya Magonjwa ya Dharura, Idara ya Mionzi, sehemu mpya ya Wagonjwa Waliopo Chini ya Uangalizi Maalum (ICU), ambayo inafanyiwa ukarabati na wodi mojawapo.
Akiwa katika Idara ya Mionzi, Dk. Kigangwala aliona jinsi mashine za MRI na CT –Scan zinavyofanya kazi.
Akizungumzia kuhusu mashine ya CT-Scan, Mkuu wa Idara ya Mionzi, Dk. Flora Lwakatare, alisema mashine hiyo mpya iliyotengenezwa na Kampuni ya Siemens, imefungwa siku mbili zilizopita na imeshaanza kufanya majaribio kwa wagonjwa 26 tangu ilipofungwa.
Dk. Flora alisema mashine hiyo ipo moja hapa nchini na katika nchi za Afrika Mashariki na kwamba nchi nyingine iliyonunua mashine hiyo ni Kenya katika Hospitali ya Aga Khan.
“Mashine hii inatoa huduma za hali ya juu kwa magonjwa ya moyo, ubongo, tumbo, kifua na ina uwezo wa kupima kifua na tumbo kwa sekunde sita,” alisema.
Akizungumzia kuhusu mashine hiyo, Dk. Kigwangalla alisema imenunuliwa kwa fedha za serikali na si mkopo na kwamba wanatarajia kununua mashine kama hiyo katika hospitali ya Dodoma na Mwanza.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa MNH, Profesa Laurence Maseru, alisema mashine hiyo ina sahani 128, mara mbili ikilinganishwa na iliyokuwepo ambayo ilikuwa inatumia sahani sita.
Kwa upande wa mashine ya MRI, ambayo ilifanyiwa matengenezo makubwa Novemba 26, mwaka jana, hadi sasa imehudumia wagonjwa 560.
Dk. Kigwangalla alitembea katika idara ya huduma za dharura na kuangalia jinsi huduma zinavyotolewa, ambapo alielezwa na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura, Dk. Juma Mfinaga, kwamba inahudumia wastani wa wagonjwa 300 hadi 400 kwa siku na kwamba kifaa hicho kinafanyakazi kwa kutumia mfumo maalum wa kompyuta bila kutumia karatasi.
Naibu waziri huyo alitoa maagizo kwa uongozi wa hospitali hiyo kuboresha huduma zinazotolewa hospitalini hapo kuwa za kitaifa zaidi.
Pia, aliutaka uongozi huo kuhakikisha unawalipa wafanyakazi fedha za malipo ya ziada kwa wakati ifikapo Februari 25, mwaka huu, kutumia mfumo wa kompyuta sehemu zote, kupunguza msongamno wa wagonjwa na kuwa wabunifu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment