MAHAKAMA
Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Ardhi, imetoa siku 60 kwa wakazi zaidi ya
681 wa Manispaa ya Kinondoni, kujitathmini iwapo wanaweza kufungua kesi ya
kupinga bomoa bomoa na wakishindwa kufanya hivyo katika muda huo, serikali
inaweza kuendelea na kubomoa nyumba zao.
Jaji
Penterine Kente, alitoa uamuzi huo jana, ambao ulikuwa unasubiriwa kwa hamu na
wakazi hao kutokana na maombi yaliyokuwa yamewasilishwa na wakazi saba,
wakiomba waruhusiwe kufungua kesi kwa niaba ya wenzao 674.
Wakazi
hao waliowasilisha maombi hayo namba 822 dhidi ya Manispaa ya Kinondoni,
Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG).
Akisoma
uamuzi huo uliochukua takriban saa moja, Jaji Kente alisema mahakama imekubali
maombi ya wakazi hao saba kwa niaba ya wenzao baada ya kupitia hoja za pande
zote husika.
Jaji
Kente alisema mahakama hiyo inatoa muda wa siku 60 kwa wananchi hao
kujitathmini kama wanaweza kufungua kesi ya kupinga bomoa bomoa ama la.
Alisema
kukubaliwa kwa ombi hilo kunatokana na mahakama kufuata misingi ya haki na
ubinaadamu kutokana na wakazi hao kushindwa kutimiza baadhi ya masharti
yaliyotolewa.
Jaji
huyo aliyataja masharti hayo kwamba ni kama waombaji hao wanaonyesha wana kesi
dhidi ya serikali, kuna uzito wa kufungua kesi hiyo kwa misingi ya haki, kwamba
inaangukia wapi sambamba na kama waombaji watapata hasara isiyopingika.
Katika
masharti hayo, Jaji Kente alisema waombaji wamekidhi sharti la kwamba watapata
hasara isiyopingika kutokana na kuvunjiwa nyumba zao.
Jaji
huyo alisema baada ya kuisha siku 60, zilizotolewa kwa waombaji hao, serikali
inaweza kuendelea na bomoabomoa mara baada ya kuisha siku hizo Machi 27, mwaka
huu.
Alisema
serikali inaweza kuendelea na bomoabomoa kama kawaida, endapo waombaji hao
watakuwa hawafungua kesi ya msingi, kikubwa ifuate misingi ya haki na sheria
katika utekelezaji wake.
No comments:
Post a Comment