Wednesday, 27 January 2016

NAIBU SPIKA AGEUKA MWALIMU WA KANUNI BUNGENI





NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Akson, jana, alipata wakati mgumu na kulazimika kusimama mara kwa mara kusoma vifungu vya kanuni, ambavyo vinawataka wabunge kutotumia lugha za kuudhi na kudhihaki jina la Rais wakati wanapochangia jambo lolote.

Aidha,  Naibu Spika pia alilazimika kutumia muda mwingine kuwaonya wabunge hao wasitumie lugha inayodhihaki watu wengine.

Mbali na hilo, aliwaasa wabunge kuheshimiana wanapochangia badala ya kuzomeana kwani hakuleti picha mzuri.

Dk.Tulia alisema hayo jana, bungeni mjini hapa, wakati wabunge walipokuwa wakichangia hutuba ya Rais Dk. John Magufuli, aliyoitoa Novemba, mwaka jana, wakati akizindua bunge.

Wakati wakichangia hotuba hiyo, baadhi ya wabunge walikuwa wakitumia lugha za kuudhi na kumdhihaki rais kinyume na kanuni.

Akichangia mjadala huo, Haji Khatibu Kai (CUF), alidai kuwa mwaka 1995 hadi 2015, wamekuwa wakidhulumiwa na serikali kwa kuibiwa kura.

Aliendelea kudai kuwa wakati Rais Magufuli alipokwenda Zanzibar kuhudhuria sherehe za Mapinduzi za Zanzibar, alikwenda huko kutangaza tarehe ya uchaguzi.

Kauli hiyo ilimfanya Dk.Tulia kusimama na kusoma kanuni za bunge, ambapo aliwataka wabunge kutotumia lugha za kuudhi na kudhihaki kwa  rais wakati wanapochangia jambo lolote.

"Kanuni ya 64 1 (d), inazungumzia kutotumia vibaya jina la rais kwa dhihaka na pia kifungu G, kinasema haipaswi kutumia lugha inayodhihaki watu wengine," alisema.

Mbunge wa Jimbo la Jang'ombe, Ali Hassani King, alisema Rais Magufuli alishughulikia mgogoro wa Zanzibar kwani aliwaita viongozi wote na hatimaye uchaguzi ulitangazwa.

Alisema Zanzibar kuna hali ya amani na utulivu, tofauti na inavyoelezwa na baadhi ya watu kuwa hakuna amani.

King alisema kuna baadhi ya watu wanadai wanataka mamlaka kamili na kwamba wamefika Marekani, Uingereza na Vatican kudai mamlaka hiyo.

Alisema mamlaka kamili ya Zanzibar yapo kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), ambayo tayari imetangaza tarehe ya uchaguzi.

Balozi Adadi Rajabu, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Muheza, alisema Rais Magufuli ameanza vizuri na kwamba, anaomba maji yapelekwe vijijini.

Mbunge wa Nkasi, Ali Kessy alisema hotuba ya Rais Magufuli imejaa mambo mazuri na kwamba, anampongeza kwa kufuta sherehe za Uhuru na anamuomba afute sherehe za Mwenge wa Uhuru.

Aliitaka serikali ipunguze majimbo kwani yamekuwa mengi na mengine yana idadi ndogo ya watu hadi 2,000, wakati kuna majimbo yana idadi kubwa zaidi ya hiyo.

No comments:

Post a Comment