NAIBU Katibu
Mkuu wa CCM (Bara) , Rajab Luhwavi, amewatahadharisha wana CCM na wananchi kwa
ujumla, kufuatia uwepo wa mtu anayetumia jina lake kutapeli wananchi.
Luhwavi
ametoa tahadhari hiyo, kufuatia malalamiko ambayo ameyapokea kutoka kwa wana
CCM na wananchi dhidi ya mtu huyo anayetumia simu ya mkononi yenye namba 0788
472076.
Akizungumza
jana na gazeti hili, Luhwavi, alisema mtu huyo ambaye anajiita Rajab Luhavi,
amekuwa akiwalaghai wanaCCM wanaowania kujaza nafasi zilizo wazi za Wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na Uenyekiti wa CCM Mkoa ambazo mchakato wake unaendelea.
Kwa mujibu
wa Luhwavi, mtu huyo amekuwa akiomba fedha kutoka kwa wanasiasa hao, kwa madai kwamba
atawasaidia katika mchakato huo ili majina yao yaweze kurudi.
Luhwavi alisema
CCM haina utaratibu huo na kuwataka wanaCCM kutambua kwamba jambo hilo
linaamuliwa na vikao ngazi za Chama na si vinginevyo.
Akifafanua Naibu
Katibu Mkuu, alisema hii ni mara ya pili kwa tukio hilo kujitokeza na kwamba
kwa mara ya kwanza ilikuwa kipindi cha mchakato wa uchaguzi mkuu, uliofanyika
Oktoba mwaka huu.
Luhwavi
alisema baadhi ya wanaCCM walibaini jina analotumia mtu huyo, baada ya kujaribu
kumtumia fedha kupitia simu yake ya mkononi.
Alisema
tayari ameshatoa taarifa polisi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na
kuwataka wanaCCM na wananchi kwa ujumla kuchukua tahadhari dhidi ya mtu huyo.
No comments:
Post a Comment