KASI ya wakurugenzi na watendaji wengine wa taasisi
na mamlaka za serikali kutumbuliwa majipu, imezidi kupamba moto, ambapo safari
hii rungu limetua ndani ya Manispaa ya Dodoma.
Jana, Waziri wa TAMISEMI, George Simbachawene, alitangaza
kumvua madaraka Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Augustino Kalinga na
kumsimamisha kazi Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu wa Manispaa hiyo na kumpa onyo kali
Ofisa Elimu Msingi wa Manispaa.
Watendaji hao wanatuhumiwa kushindwa kusimamia na kutekeleza
waraka wa utoaji wa Elimu Bure.
Akizungumza mjini hapa jana, Simbachawene alisema amefikia
uamuzi huo kutokana na kubainika wazazi kuchangishwa michango ya mlinzi, umeme
na maji, ambayo ni kinyume cha agizo na azma ya serikali ya kutoa elimu bure.
Alisema Kalinga amevuliwa madaraka yake kuanzia jana,
kutokana na kubainika kushindwa kuwasimamia watumishi walio chini yake hadi kusababisha
kuandika na kusambaza barua kwa walimu wakuu wa shule za msingi Manispaa ya
Dodoma.
Alisema hiyo inakwenda kinyume na maelekezo ya serikali
yaliyo kwenye mwongozo na ameshindwa pia kusimamia utekelezaji wa maelekezo
sahihi ya serikali kuhusu utoaji wa elimu ya msingi bila malipo.
"Kutokana na kasoro hizo na kwa mamlaka
niliyonayo, namvua madaraka kuanzia leo tarehe 25/1/2016," alisema
Simbachawene.
Kwa upande wa Ofisa Elimu Vifaa na Takwimu Msingi wa
Manispaa ya Dodoma, Josephine Akimu, alisema amemsimamisha kazi kwa kosa la
kudharau maekezo ya kiongozi wake, kutia saini barua kwa niaba ya mkurugenzi
huku akitumia jina la Ofisa Elimu wake bila ridhaa yake.
Alisema uamuzi huo unalenga pia kupisha uchunguzi
dhidi yake, ikiwemo kufahamu uwezo wake kiutendaji.
Akizungumzia Ofisa Elimu Msingi wa Manispaa ya
Dodoma, Scola Kapinga, alisema anapewa onyo kwa kosa la kutokuwa makini na
idara yake hadi kusababisha barua hiyo kuandikwa na kusambazwa katika shule
zote za msingi zilizopo ndani ya manispaa hiyo bila yeye kuwa na taarifa.
Simbachawene alitumia fursa hiyo kuwaagiza wakuu wa
mikoa, makatibu tawala wa mikoa, wakuu wa wilaya, na wakurugenzi wa mamlaka za serikali
za mitaa kuendelea kuwaelimisha wakuu wa shule za msingi na sekondari katika
maeneo yao ili kupata uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa elimu bure.
Pia, kufanya ufuatiliaji katika maeneo waliyopo
kuhakikisha maelekezo ya utoaji wa elimu ya msingi bila malipo inatekelezwa
kama ilivyokusudiwa.
Januari 22, mwaka huu, Waziri Simbachawene
alimuagiza Katibu Mkuu, TAMISEMI (Elimu), kumuita ofisini mara moja mkurugenzi
pamoja na watendaji wote wanaohusika na idara ya elimu, akiwemo ofisa elimu
ili waweze kutoa maelezo ya kina ni kwanini wameandika barua hiyo na msingi
wake ulikuwa nini, wakati serikali imeshatoa fedha ambazo zinapaswa kufanya
kazi hiyo.
Baada ya viongozi hao kuitwa na kutoa maelezo,
ilibainika kuwa kuna kasoro na hivyo kumlazimu waziri kuchukua hatua kama
alivyokuwa ameahidi baada ya kufika shule ya msingi Makulu na kukuta wazazi
wakiombwa kuchangia fedha ya umeme, maji na mlinzi.
Simbachawene alisema kuwa hatua hiyo iliyochukuliwa
ni ya kwanza, uchunguzi unaendelea.
No comments:
Post a Comment