SERIKALI
imesema itawachukulia hatua za kisheria watendaji wa halmashauri wanaotumia
fedha nyingi kwa ajili ya kupambana na ugonjwa kipindupindu, lakini ugonjwa huo
bado upo kwenye halmashauri zao.
Aidha,
imesema hadi mwezi Machi, mwaka huu, wanataka ugonjwa huo uwe umemalizika
kwenye maeneo yote.
Mbali
na hilo, imesema tangu ugonjwa huo ulipoingia hadi sasa, imetumia takribani sh.
bilioni moja kwa ajili ya kupambana nao.
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema
hayo jana, alipokuwa akitoa taarifa ya ugonjwa wa kipindupindu katika kipindi
cha wiki moja, Bungeni mjini Dodoma.
Alisema
wanafikiria kuwawajibisha watendaji wa halmashauri, ambao wanatumia fedha
nyingi kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa kipindipindu, lakini wameshindwa kuudhibiti
kwenye maeneo yao.
Ummy
alisema wizara hiyo imeweka mikakati kuwa ifikapo Machi, mwaka huu, ugonjwa huo
uwe umemalizika kwenye maeneo yote.
Alisema
hadi kufikia juzi, watu 14,608 wameugua ugonjwa huo, kati yao watu 228,
wamefariki dunia na kwamba mikoa ya Njombe, Ruvuma na Mtwara ndio pekee ambayo
haijawahi kuripoti mgonjwa yoyote wa kipindupindu.
Ummy
alisema mikoa 15, imeripoti kuwa na wagonjwa wa kipindupindu, ambapo idadi ya
wagonjwa kwenye mikoa hiyo ni 524 na vifo vilivyoripotiwa ni 10.
Hata
hivyo, alisema mkoa wa Morogoro bado unaendelea kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa,
ikilinganishwa na mikoa mingine na kwamba, mkoa wa Dar es Salaam, hauna mgonjwa
yoyote katika kipindi cha mwezi mmoja sasa.
Ummy
alizitaja manispaa zenye wagonjwa kuwa ni Morogoro (89), Halmashauri ya
Morogoro (36), Mvomero (17), Ukerewe (36), Nyamagana (19), Ilemela (13) mkoani
Mwanza, Bariadi (29), Bariadi Manispaa (23) mkoani Simiyu.
Mikoa
mingine yenye wagonjwa wa kipindupindu ni Manyara, Mara, Geita, Mbeya, Dodoma,
Arusha, Tabora, Singida, Lindi, Rukwa, Kilimanjaro na Kagera.
Ummy
alizitaka mamlaka za mikoa, halmashauri pamoja na watendaji, kuendeleza juhudi
za kuzuia kusambaa kwa mlipuko wa ugonjwa huo.
Alisema
ugonjwa wa kipindupindu bado upo, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kuzuia
ugonjwa huo.
Ummy
alisema wizara hiyo inaangalia kufanya marekebisho ya sera ya afya, ambayo ni
kuzuia badala ya kutibu ugonjwa huo.
No comments:
Post a Comment