KAZI ya kutumbua majipu iliyoanzishwa na Rais John
Magufuli, imeendelea kushika kasi na safari hii imebisha hodi katika Mamlaka ya
Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Rais Magufuli amebisha hodi NIDA kwa kutengua uteuzi
wa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Dickson Maimu kuanzia jana.
Baada ya utenguzi huo, Rais Magufuli amesimamisha
kazi Maimu ili kupisha uchunguzi kuhusu tuhuma dhidi yake.
Mbali na Maimu, Rais Magufuli pia amewasimamisha kazi
maofisa wengine wanne wa NIDA. Maofisa hao ni Mkurugenzi wa TEHAMA, Joseph
Makami; Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande; Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina Nyoni na
Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.
Mbali na kusimamishwa kazi kwa maofisa hao wa NIDA,
Rais Magufuli pia ameagiza kurejeshwa nyumbani mara moja, mabalozi wawili,
ambao mikataba yao imekwisha.
Mabalozi hao ni Batilda Buriani, aliyeko Tokyo, Japan
na Dk. James Msekela, aliyeko Rome, Italia. Pia amemrejesha nyumbani Balozi wa
Tanzania, aliyeko London, Uingereza, Peter Kallaghe, ambaye amerejeshwa Wizara
ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa,
atakakopangiwa kazi nyingine.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, mjini Dar
es Salaam jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, alisema Rais Magufuli
amefikia uamuzi huo kutokana na ripoti zilizomfikia kuonyesha kuwa, NIDA hadi
sasa imetumia sh. bilioni 179.6.
“Kiasi hiki ni kikubwa na Rais angependa ufanyike
uchunguzi na ukaguzi jinsi fedha hizo zilivyotumika, maana Rais amekuwa
akipokea malalamiko ya wananchi kuhusiana na kasi ndogo ya utoaji wa vitambulisho
vya Taifa.
“Hivyo Rais ameelekeza Mamlaka ya Udhibiti wa
Manunuzi ya Umma (PPRA), wafanye ukaguzi maalumu wa manunuzi yote yaliyofanywa
na NIDA, “alisema Balozi Ombeni.
Aliongeza kuwa, Rais Magufuli pia ameelekeza Mdhibiti
na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, afanye ukaguzi maalumu wa hezabu za NIDA,
ikiwemo ukaguzi wa ‘Value for money’, baada ya kuthibitisha idadi halisi ya
vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa.
Aidha, Balozi Sefue alisema Rais Magufuli pia
ameelekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ifanye
uchunguzi kujiridhisha kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au la.
Kuhusu mabalozi Batilda na Msekela, waliorejeshwa
nchini, Balozi Sefue alisema wanatakiwa kukabidhi kazi kwa ofisa mkuu au
mwandamizi aliye chini yao.
Kutokana na maagizo hayo ya Rais Magufuli, vituo vya
ubalozi vilivyo wazi kwa sasa ni Uingereza, Ubelgiji, Italia, Japan, Malaysia
na Brazil.
Ubalozi wa Ubelgiji upo wazi, kufuatia aliyekuwa Balozi Dk. Deodorous
Kamal, kuchaguliwa kuwa mbunge, ubalozi wa Malaysia upo wazi kutokana na
aliyekuwa Balozi Dk. Azizi Ponray kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo
ya Nje wakati ubalozi wa Brazil upo wazi kutokana na Balozi Francis Malambugi
kustaafu.
Aidha, Balozi Sefue alisema Rais Magufuli amemteua
aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika
serikali ya awamu ya nne, Mahadhi Juma Mahadhi, kuwa balozi wa kwanza wa
Tanzania nchini Kuwaita, kufuatia uamuzi wa serikali kufungua ofisi za ubalozi
nchini humo.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli ametengua uteuzi
wa Injinia Juma Kipande kabla hajathibitishwa kuwa Katibu Tawala wa mkoa wa
Katavi kutokana na utendaji usioridhisha.
Balozi Sefue alitumia fursa hiyo kuwahimiza viongozi
wote wa utumishi wa umma, kubadilika kwa dhati kwenye utendaji wao na uadilifu.
“Napenda kusisitiza kuwa Rais na sisi tunaomsaidia
hatuoni raha kuchukua hatua dhidi ya viongozi na watumishi wengine. Tungependa
kila mtu ajirekebishe na kutomfikisha Rais mahali ambapo inabidi amchukulie
hatua,”alisema.
Ametaka kila kiongozi na mamlaka ya nidhamu isipate
kigugumizi kusimamia utendaji na maadili ya kazi, kila mamlaka isipate
kigugumizi kuchukua hatua za nidhamu, lakini ifanye hivyo kwa kuzingatia kwa
ukamilifu sheria, kanuni na taratibu katika utumishi wa umma.
Aidha, ameagiza lazima uongozi na watumishi wa umma,
wawahudumie wananchi kwa haki, weledi,
uadilifu na heshima na kwamba, kila ofisi ya serikali iwe na dawati la
kusikiliza shida za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Balozi Sefue pia ameagiza kwenye ofisi ya mkuu wa
mkoa na wilaya, wajenge uwezo wa kushughulikia shida za wananchi kwa ukamilifu
na wakati ili wasikimbilie kwenda Ikulu.
Pia, ameagiza kuanzia sasa watumishi wote wa umma
wavae beji zenye majina yao ili iwe rahisi kwa mwananchi kumtambua anayemhudumia.
No comments:
Post a Comment