MWENYEKITI Mwenza wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (UKAWA), Freeman Mbowe, amesema kuna mkakati mbadala kuhusu mgogoro wa
kisiasa Zanzibar, ambao utatangazwa baada ya kikao cha Baraza Kuu la chama cha
CUF.
Mbowe alisema hayo jana, Bungeni
mjini hapa na kuongeza kuwa, mkakati huo utatangazwa Januari 28, mwaka huu,
baada ya kikao cha kamati tendaji cha baraza hilo kitakachokutana Januari 27,
mwaka huu.
Alisema wameamua kuja na mkakati huo
baada ya kufanya mazungumzo ya mashauriano kuhusiana na hali ya kisiasa ya
Zanzibar, baada ya kupokea taarifa ya mazungumzo ya awali yaliyofanyika kati ya
Maalim Seif Sharif Hamad na serikali, ambayo hayakufikiwa muafaka.
Mbowe alisema: “Sisi tutaunga mkono
msimamo wa baraza hilo na kikao hicho ndicho kitakachotoa muelekeo wa siasa
gani tufanye, kwa sababu tumeshaona serikali ya CCM na wenye maamuzi wanataka
kutuyumbisha, hivyo ni vyema wakatambua kuwa amani ya taifa haiwezi kudumu kama
haki haitazingatiwa.”
Alisema haki haiwezi kupatikana kwa
vitisho bali maamuzi ya wananchi yatakapoheshimiwa na kwamba Rais John Magufuli
hapaswi kujitoa kwa namna yoyote kwa sababu ndiye amiri jeshi mkuu na majeshi.
Mnadhimu Mkuu wa kambi ya upinzani
Bungeni, Tundu Lissu alisema hawana mpango wa kulipeleka suala hilo mahakamani
kwani linapaswa kumalizwa kisiasa.
Alisema suala la mgogoro wowote
unaohusisha matokeo ya urais, kisheria hauruhusiwi kupingwa katika mahakama
yoyote ile kwa mujibu wa katiba.
Lissu alisema njia pekee iliyobaki
ya kumaliza mgogoro huo ni ya kisiasa na kwamba, matokeo ya uchaguzi wa
Zanzibar, yalifutwa na mtu ambaye hamna mamlaka ya kikatiba ya kufanya hivyo.
Mbunge wa Jimbo la Malindi, Ali
Salehe, alisema iwapo watarudia ama kutorudia uchaguzi, CUF haiwezi kujimaliza
kisiasa. Alisema Rais Magufuli anayo nafasi kubwa ya kuingilia kati mgogoro huo.
No comments:
Post a Comment