KAMBI ya upinzani Bungeni, imesema bado kuna mvutano baina yake na ofisi ya Spika kuhusu mgawanyo wa wajumbe wa kamati, ikiwemo Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Hesabu Serikali za Mitaa (LAAC), Kamati ya Nishati na Madini na Katiba na Sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari
mjini hapa, jana, Kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema
kwa mujibu wa kanuni za bunge, Spika ana mamlaka kikanuni, kuunda kamati.
Mbowe alisema kanuni zimeainisha
vigezo atakavyotumia spika katika kuunda kamati hizo, ambavyo ni chaguo la
wabunge, kwa kujaza fomu na kuchagua kamati wanazozitaka, sifa halisi ya
kamati, mgawanyiko wa kivyama.
“Tunavyosema Spika hatuzungumzii mtu
bali ni ofisi, ambayo yupo katibu wa bunge na wasaidizi, hivyo katika kuunda
kamati hizo, haundi Spika pekee yake, licha ya kutumia vigezo vinavyotakiwa,”
alisema.
Alisema baada ya majina ya wajumbe
wa kamati kutangazwa, walibaini kutotumika vigezo hivyo wakati wa kupanga
kamati na kwamba, katika majina yaliyoteuliwa, hakukuwa na dhamira njema bali
kulikuwa na mkakati wa kuwapangua wabunge wa kambi hiyo, wenye uzoefu na uwezo
kulingana na kamati husika walizochagua.
Akitolea mfano wa kamati hizo, Mbowe
alidai kuwa ni pamoja na PAC na LAAC, ambazo zinapaswa kuongozwa na wapinzani,
lakini kumekuwa na ukandamizaji wa ofisi ya Spika kuwanyima uhuru wapinzani kwa
kuwachagulia wagombea.
“Bado mvutano unaendelea, sisi tuna kanuni
zinazotuongoza, lakini bunge limetumika kukandamiza wapinzani na kutuchagulia
wawakilishi wanaowataka wao, wakati tunaweza kuzijaza wenyewe kwa sababu
tunajua nani ana uwezo wa kuongoza kulingana na taaluma,” alisema.
Alisema kambi ya upinzani inaamini
kama kanuni inawataka kuongoza kamati hizo, ilipaswa wapewe nafasi na uhuru
katika kulisimamia jambo hilo.
Akizungumzia kamati ya sheria,
alitolea mfano kuwa mnadhimu wa kambi ya upinzani, Tundu Lissu, ameachwa kwenye
kamati hiyo.
Mbowe alisema wamepangiwa kamati
ambazo mchango wao katika kulisaidia taifa hautaonekana.
Kuhusu kamati ya madini na nishati, Mbowe
alisema imeundwa na wajumbe wapya, wakati kamati hiyo inagusa rasilimali za
taifa.
Alisema katika mazingira hayo,
hawako tayari kukubaliana na uamuzi huo na kwamba, serikali ikae na kuamua
katika kambi yao nani awe kiongozi ila kama wamepewa madaraka waachiwe majukumu
hayo.
No comments:
Post a Comment