SERIKALI imesema itabaki kama
mshauri katika mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar kwa sababu wananchi wenyewe ndiyo
wenye uwezo wa kuutatua.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.
Philip Mpango, alisema hayo jana, alipokuwa akijibu hoja za wabunge, baada ya
kumaliza kuchangia mjadala wa mapendekezo ya mwelekeo wa mpango wa pili
wa maendeleo wa miaka mitano.
Dk. Mpango alitoa ufafanuzi huo,
baada ya mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, kueleza namna mpango huo unavyozungumzia
amani, usalama, umoja, haki na demokrasia, mambo ambayo amedai hayapo
kiuhalisia kutokana na serikali kushindwa kumaliza mgogoro wa Zanzibar.
Mbowe alidai kuwa mipango hiyo
haitekelezeki kwa sababu ya serikali inataka kutumia nguvu ya kupora ushindi wa
rais aliyepatikana.
Hata hivyo, Dk. Mpango alisema
mgogoro wa Zanzibar, utamalizwa na wananchi na Serikali ya Zanzibar na Tanzania
Bara itabaki kuwa mshauri.
Akizungumzia mpango huo wa mwaka
2016/2017, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashantu Kijaji, alisema unakusudia
kuwa na viapaumbele vinne, ambavyo ni viwanda vya kuimarisha kasi ya uchumi na
miradi mikubwa ya kielelezo ya kuwezesha uchumi kupaa.
Vipaumbele vingine ni miradi
inayoendelea hususan ya maeneo wezeshi, ikiwemo barabara, reli, bandari, maji
na mawasiliano kwa maendeleo ya viwanda na maeneo yatakayolenga kufungamanisha
maendeleo ya viwanda na maendeleo ya watu.
Wakichangia kuhusu mpango huo,
baadhi ya wabunge walidai hauwezi kutekelezeka kutokana na kuwa hauna uhalisia
kwani mambo mengi yaliyoandikwa, likiwemo suala la maji vijijini, limetajwa
kuwa yanapatikana kwa asilimia 68 mijini na kudai kuwa si kweli kutokana na
maeneo mengi hayana maji.
Waliitaka serikali kuorodhesha kwa
kutaja maeneo, ambayo maji yanapatikana na kwa kiasi gani.
Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya,
alisema katika jimbo lake, hakuna maji hata kidogo na anashangazwa kusikia maji
yanapatikana kwa asilimia 68.
Aliishauri serikali kutafuta namna
ya kukusanya maji ya mvua ili yaweze kuwasaidia wananchi waweze kushiriki
katika kilimo cha umwagiliaji na pia zijengwe reli nyingi ili kusaidia barabara
nyingi zisiharibike.
Mbunge wa Babati, Jitu Son alisema
taifa halifanikiwi kwenye mipango linayopanga, hususan kwenye sekta ya kukua
kwa viwanda, kutokana na kuwepo kwa tozo nyingi na kodi.
Alisema asilimia 78 ya mbegu
zinatoka nje ya nchi na wanazichukua kutokana na wanaozalisha mbegu wanatozwa
tozo 26, hivyo ameomba tozo hizo zipunguzwe na wapandishe kodi za watakaoagiza
kutoka nje ili wafanyabiashara waweze kutumia zinazozalishwa nchini.
Husein Bashe, mbunge wa Nzega Mjini,
alisema kilimo kinaporomoka nchini na kushauri Benki ya Kilimo, iwezeshwe na kuwasaidia
wakulima ili waweze kulima zaidi na kwamba asilimia 10 ya bajeti ipelekwe
kwenye kilimo.
Akijibu hoja hizo, Dk. Mpango
alisema wamepokea mapendekezo yote na kuyafanyia kazi kadri itakavyowezekana.
Alisema takwimu zote hususan za maji,
ambazo wabunge wamezilalamikia kuwa hazina uhalisia kutokana na maeneo mengi
kukosa maji, wanazipata kutoka ngazi za chini.
No comments:
Post a Comment