WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa
Makame Mbarawa, amemteua Mhandisi George Sambali, kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Mhandisi Sambali, ambaye alikuwa Mkurugenzi wa
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), anakaimu nafasi hiyo
kutokana na kifo cha Mhandisi Suleiman Suleiman, aliyefariki Januari 18, mwaka
huu.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, anayeshughulikia sekta
ya uchukuzi, Dk. Leonard Chamuliho, alisema uteuzi huo
ulianzia Januari 20, mwaka huu.
Mhandisi Sambali alizaliwa mwaka 1965, mkoani
Tabora na ana shahada ya uzamili ya sayansi ya uhandisi, uchukuzi na barabara,
aliyoipata mwaka 2001, nchini Uholanzi.
Mhandisi Sambali alihitimu shahada ya kwanza ya
Sayansi ya Uhandisi Ujenzi katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1995.
Pia, amepata mafunzo na kozi mbalimbali za masuala
ya anga kutoka katika vyuo vya hapa nchini na nje ya nchi, ikiwemo Stashahada
ya Uongozi wa Viwanja vya Ndege mwaka 2014 huko Montreal, Canada.
Mwaka 2015, alitunukiwa Stashahada ya Wataalamu wa
Kimataifa wa Viwanja vya ndege chini ya AMPAP nchini Canada.
Mhandisi Sambali aliajiriwa na TAA mwaka 2001, kama
Meneja Mipango, Usanifu na Uthamini na mwaka 2012, aliteuliwa kuwa Kaimu
Mkurugenzi wa Huduma za Uhandisi na Ufundi.
Mwaka 2013, Mhandisi Sambali aliteuliwa kuwa
Mshauri Maalumu wa Mkurugenzi Mkuu kabla ya mwishoni mwa mwaka jana, kuteuliwa
tena kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha JNIA.
No comments:
Post a Comment