Tuesday, 26 January 2016

MWANAHARAKATI APINGA NDOA ZA UTOTONI KORTINI






MWANAHARAKATI wa Haki za Binaadamu, Rebecca Gyumi, amefungua kesi ya Kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, akipinga vifungu vya Sheria ya Ndoa vinavyotoa ruhusa kwa mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 14, kwa kibali cha mahakama na 15 kwa ridhaa ya wazazi.
Pia, anaiomba mahakama hiyo, kupandisha umri wa chini wa kuoa ama kuolewa kwa wanaume na wanawake kuwa miaka 18.
Rebeca, ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Msichana  Initiative, alifungua kesi hiyo jana, iliyopewa namba tano ya mwaka huu, kwa kupitia wakili wake, Jebra Kambole.
Kwa kupitia hati ya madai, mwanaharakati huyo anaiomba Mahakama Kuu kuvifuta baadhi ya vifungu vilivyoko katika Sheria ya Ndoa.
Mwanaharakati huyo anaiomba mahakama hiyo kuvifuta vifungu vya  13 na 17 vya Sheria ya Ndoa kwa kutoa mwanya kwa watoto wa kike kuolewa wakiwa na miaka  14, kwa kibali cha mahakama.
Pia, miaka 15 kwa ridhaa ya wazazi, jambo ambalo anadai ni kinyume na Ibara ya 13, 12 na 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, ambavyo vinatoa haki ya usawa mbele ya sheria, kutokubaguliwa, kuheshimu utu wa mtu na uhuru wa kujieleza.
Kwa mujibu wa wakili huyo, vifungu hivyo katika Sheria ya Ndoa, vimeweka umri tofauti kati ya mtoto wa kike na kiume, hivyo kupingana na Ibara ya 13(1)(2) ya Katiba, inayotoa haki ya usawa mbele ya sheria.
Alidai ni kosa kuwa na sheria zinazobagua na kuendelea kudai kwamba, wakati mtoto wa kike anaweza kuolewa katika umri huo, mtoto wa kiume anatakiwa kuoa akiwa na miaka 18.
Wakili huyo anadai kifungu cha 17 cha Sheria ya Ndoa, ambacho kinatoa ruhusa kwa mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 15, kwa ridhaa ya wazazi wake, kinaminya utu na haki ya mtu kujieleza.
Alidai haki hizo zimeainishwa katika Ibara ya 12 na 18 ya Katiba na kwamba, masuala ya ndoa sio kama mikataba ya biashara, pande zinazoingia kwenye ndoa lazima zikubalike na si kulazimishwa.
Wakili huyo alidai kuna matukio ya baadhi ya wazazi kukatisha mtoto wa kike masomo ili aweze kuolewa.  Shauri hilo limepangwa Alhamisi wiki hii.
Akizungumza nje ya mahakama, Rebeca alidai ndoa za utotoni kwa mtoto wa kike, mbali ya kukiuka haki za binadamu, pia zinahusu masuala ya kiafya, kielimu na kisaikolojia.
Alidai msichana anayejifungua akiwa na umri mdogo, imekuwa ni chanzo cha matatizo ya vifo vingi vya wajawazito na fistula.

No comments:

Post a Comment