Na Felix Mwagara
SERIKALI imeagiza kuchukuliwa
hatua kali kwa askari polisi wote wenye tabia ya kuwabambikizia kesi raia.
Agizo hilo limetolewa na Katibu
Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira,
ambapo amewataka viongozi wakuu wa Jeshi la Polisi kuhakikisha tabia hizo
zinakomeshwa.
Meja Jenerali Rwegasira alisema
jeshi hilo lina sifa nzuri nje ya nchi pamoja na hapa nchini, lakini kuna
baadhi ya askari wasio waadilifu wanawaonea wananchi mitaani wasiokuwa na
hatia.
“Jeshi letu lina sifa nzuri,
niliwahi kwenda nchini Kenya nikaambiwa Jeshi la Polisi Tanzania lina maadili
kwani hata likimkamata mhalifu, linafuata sheria na utaratibu na sio kutumia
nguvu kubwa kama yalivyo majeshi mengine,” alisema Rwegazira.
Aliongeza kuwa amefurahishwa na
utendaji kazi wa jeshi hilo na kutaka kuongeza umakini zaidi ili kuliletea sifa
zaidi. Alisema binafsi yupo karibu nao katika kuliendeleza jeshi hilo ili
liweze kufanya kazi kwa weledi.
Alisema ni askari wachache mno
wenye tabia hiyo ya kuwabambikizia kesi wananchi na kutofuata sheria za jeshi,
hivyo kazi ya kupambana na askari hao inawezekana endapo viongozi wa jeshi
wakiamua kulifanyia kazi.
“Utendaji kazi wenu ni mzuri,
nawapongeza sana hasa mlivyosimamia uchaguzi mkuu vizuri kwani wananchi wengi walikuwa
na wasiwasi kuhusu usalama wao katika kipindi cha uchaguzi, lakini mlisimama
imara kuhakikisha uchaguzi unamalizika salama,” alisema Rwegasira.
Mkuu wa Jeshi hilo nchini, IGP
Ernest Mangu, aliwapongeza viongozi hao wa wizara kwa kuwatembelea kwa kuwa ni
faraja kubwa kwao.
No comments:
Post a Comment