MSAJILI
wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, ameviasa vyama vya siasa
kushiriki kwenye uchaguzi utakaotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) pamoja na uchaguzi wa marudio
wa Zanzibar, utakaofanyika Machi 20, mwaka huu.
Kwa
mujibu wa barua iliyotolewa kwa vyama hivyo jana, Jaji Mutungi alisema, kimsingi
Sheria ya Vyama Vya Siasa Sura ya 258, inasisitiza vyama vya siasa
kushiriki katika chaguzi zote zinazotangazwa na tume za uchaguzi ili
kufikia malengo yake ya kushika dola.
“Ni
wajibu wa kila chama cha siasa nchini, kama wakala wa kukuza demokrasia,
utawala wa sheria na amani ya nchi, kuwa wa kwanza kutii matamko ya kisheria
yanayotolewa na mamlaka husika .
“Kama
kuna chama cha siasa hakiridhiki au kimekwazwa kwa njia moja au nyingine na
suala lolote kuhusu masuala ya uchaguzi, njia stahiki na inayoonyesha ukomavu
wa kisiasa si kuhamasisha kugomea uchaguzi, bali ni vema kikafuata utaratibu
uliowekwa katika sheria za uchaguzi,” alisema Jaji Mutungi.
Aidha,
Msajili huyo alisema kwa mujibu wa sheria za nchi, bado ni suala la hiari kwa
chama kushiriki uchaguzi, lakini utashi huo wa hiari unaenda sanjari na umuhimu
wa kila chama kushiriki kila uchaguzi unaotangazwa na tume ya uchaguzi.
“Hivyo
ni muhimu kila chama cha siasa kuelewa
kuwa, uchaguzi ni kipimo cha uhai wa chama cha siasa. Chama cha siasa
kisiposhiriki uchaguzi, kinaua uhai wake katika mtazamo wa harakati za
kisiasa,” alisisitiza.
Aliongeza
kuwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na vyama vya siasa umeimarika, hivyo
sio vyema kwa chama cha siasa kujirudisha nyuma au kujiua kisiasa kwa
kutoshiriki uchaguzi wakati kina uwezo wa kufanya hivyo.
No comments:
Post a Comment