UONGOZI wa
Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), umetangaza kuhamishia huduma zake za
usafirishaji mjini Dodoma, kuanzia keshokutwa.
Taarifa
iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Mhandisi Elias Mshana, imesema
huduma hizo zinahamishiwa kwa muda mjini Dodoma, hadi pale kazi ya ukarabati ya
tuta la reli, litakapotengemaa kati ya stesheni za Kidete na Kilosa mkoani
Morogoro.
Hata hivyo,
alisema kutokana na mafuriko ya eneo hilo, bado haijajulikana tuta hilo
litatengemaa lini.
Alisema uongozi
umeamua kwa sasa kusitisha zoezi la ukarabati ili kuokoa rasilimali
zinazotumika katika ukarabatiwa wa eneo hilo.
Hata hivyo,
alisema kazi ya kuzuia uharibifu zaidi dhidi ya tuta la reli inaendelea
kulingana na hali inavyojitokeza.
Wakati huo huo, uongozi wa TRL umeandaa utaratibu
na wamiliki wa mabasi, kuwasafirisha abiria wake watakaotumia huduma zake
zinazoanzia Jumanne na Ijumaa, mjini Dodoma, wakitokea Dar es Salaam.
TRL imesema
maombi ya huduma za kusafirisha shehena yataanza kupokelewa keshokutwa, lakini treni
ya kwanza ya abiria imepangwa kuondoka Dodoma, Februari 2, mwaka huu, saa mbili usiku.
Kwa mujibu wa
taarifa ya TRL, wananchi wanaweza kuanza kukata tiketi za safari ya Jumanne,
wakati wowote baada ya kusoma taarifa hii katika stesheni za reli ya kati zilizo karibu
yao.
TRL imesema
mabadiliko hayo ya usafiri yataongeza gharama, lakini ni muhimu kwa huduma za
usafirishaji ziendelee ili kuwasaidia Watanzania kiuchumi na kijamii kadri inavyowezekana.
Miaka ya 1998
na 2010, huduma za reli zilihamishiwa Dodoma kwa muda baada ya eneo kati ya
Gulwe, Godegode mkoani Dodoma, Kidete na
Kilosa mkoani Morogoro, kukumbwa na
mafuriko makubwa na kuisambaratisha njia ya reli.
No comments:
Post a Comment