WAKATI Rais Dk. John
Magufuli akiendeleza kasi ya utumbuaji majipu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU), imecharuka kwa kuwashushia rungu vigogo na kampuni
zilizohusika kwenye kashfa za ukwepaji kodi na ubadhirifu wa mali za umma.
Kampuni na vigogo
waliokumbwa na rungu hilo ni Kampuni ya Mafuta ya Lake Oil, vigogo waliohusika
kwenye sakata la Benki ya Stanbic, Shirika Hodhi la Reli (RAHACO) na kashfa ya
mabehewa mabovu ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).
Pia, TAKUKURU imeanza uchunguzi
kwa vigogo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), kufuatia matumizi
makubwa ya kisasi cha shilingi bilioni 179.6, ambazo licha ya fedha hizo
kutumika kwenye mradi wa vitambulisho vya taifa, bado idadi kubwa ya wananchi
hawajapata vitambulisho hivyo.
Hatua hiyo ni muendelezo
wa TAKUKURU wa kupambana na rushwa, ambapo kuanzia sasa taasisi hiyo itanza
uchunguzi mara moja kwa watumishi wote wa serikali watakaosimamishwa kazi kwa
tuhuma za rushwa.
Akizungumza na waandishi
wa habari Dar es Salaam, jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Valentino
Mlowola, ametoa onyo kwa maofisa maduhuli, wafanyabiashara, watoa huduma kwa
umma pamoja na wanachi kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa.
“Watu nataka wafahamu
kuwa, ile tabia ya kutoa na kupokea rushwa imefikia kikomo, hatutajali nafasi
ya mtu wala hadhi yake kwenye jamii,” alisisitiza Mlolowa.
KASHFA YA LAKE OIL
Kampuni hiyo ilidanganya
kusafirisha mafuta ya petrol lita
17,461,111.58, kwenda Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Kwa mujibu wa Mlowola,
Lake Oil badala ya kusafirisha mafuta hayo kwenda DRC, iliyauza kwenye soko la
ndani na kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni 8.5.
Baada ya TAKUKURU
kukamilisha uchunguzi, kampuni hiyo pamoja na washirika wake walipewa miezi
miwili kurejesha fedha hizo serikalini na endapo itashindwa kufanya hivyo,
watawafikisha mahakamani.
Kwa mujibu wa kamishna
huyo, Lake Oil imeridhia kuilipa serikali fedha hizo, ambazo serikali ililipa
hasara kufuatia kampuni hiyo kukwepa kodi.
SAKATA LA STANBIC
TAKUKURU imendeleza moto
kwenye sakata hilo linalohusu malipo ya Dola za Marekani milioni sita kwa
kampuni ya Enterprise Growth Market Advisor (EGMA).
Kampuni hiyo ililipwa
fedha hizo kwa madai ya malipo kwa kuisaidia serikali kupata mkopo wa Dola za
Marekani milioni 600.
Kampuni hiyo
ilihusika katika uwezeshaji wa upatikanaji wa mkopo wa serikali ya
Tanzania, ambao Standar Bank Plc (ambayo
kwa sasa inajulikana kama ICBC Standard
Bank) na Benki ya Stanbic kwa pamoja
walikuwa wawezeshaji wakuu (Lead Arranger).
Baada ya kumalizika kwa
uchunguzi wa serikali, ilibainika kuwa malipo ya kampuni ya EGMA yalikuwa
yamefanyika kinyume cha taratibu za kibenki na yalihusisha uongozi wa Benki ya
Stanbic.
Fedha hizo zilitakatishwa
na baadhi ya watumishi wa umma, wakishirikiana na baadhi ya watu kutoka sekta
binafsi huku wakifahamu kuwa fedha hizo wamezipata kwa njia haramu.
Mlolowa, ambaye awali
alikuwa Kamishna wa Polisi anayehusika na mapambano dhidi ya ugaidi,
alibainisha kuwa, upelelezi huo umefikia kwenye hatua nzuri na wahusika
watafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.
“Watuhumiwa wote bila
kujali hadhi au nafasi yao na taasisi zinazohusika, watachukuliwa hatua za
kisheria,” alisema.
Tayari Benki Kuu ya
Tanzania (BOT), imeitoza faini ya sh. bilioni tatu, Benki ya Stanbic, ikiwa ni
moja ya hatua zilizochukuliwa kutokana na kushiriki katika sakata hilo.
Aidha, BOT imeitaka benki
hiyo kuwasilisha utetezi wake katika kipindi cha siku 20, ambacho kitaisha
baadaye mwezi huu.
Desemba 2, mwaka jana, serikali ilimtaka kiongozi wa
Kampuni ya EGMA, Harry Kitilya, ambaye alikuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), kutoa ushirikiano kwa vyombo vya serikali kuhusu fedha
hizo.
Mbali na Kitilya, kampuni hiyo inamilikiwa na Fartern
Mboya, inadaiwa kufanya udanganyifu wa ada ya mkopo wa fedha hizo, ambazo zilipewa
serikali na benki ya Standard ya Uingereza.
Kampuni hiyo ililipwa dola milioni sita, sawa na sh.
bilioni 15, za Tanzania, kwa ajili ya malipo ya hati fungani wakati serikali
haikupaswa kulipa.
JIPU LA RAHCO
Jipu hilo,
limeshatumbuliwa na Rais Dk. Magufuli kwa kutengua uteuzi na kumsimamisha kazi,
aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Mhandisi Benhadard Tito.
Mhandisi huyo
alisimamishwa kazi kutokana na tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikimkabili, ambazo
TAKUKURU imeanza kuzichunguza.
Uchunguzi huo unahusisha
ukiukwaji wa sheria na taratibu za kuwapata wazabuni kwenye ujenzi wa reli ya
kisasa (Standard Gauge), uliokuwa ukisimamiwa na RAHCO.
Kamishna Mlowola alisema baadhi
ya watuhumiwa kwenye kesi hiyo wameshakamatwa, akiwemo raia wa Kenya, Kanji
Muhando. aliyekuwa kiungo muhimu katika mchakato wa kumpata mzabuni.
UFISADI WA MABEHEWA TRL
Kwa mujibu wa Mlowola,
shauri hilo linahusu ukiukwaji wa Sheria ya Manunuzi ya Umma pamoja na kanuni
zake, katika ununuzi wa mabehewa 25 ya kokoto kutoka kampuni ya Hindusthan
Engineering and Industries Limited.
Alisema shauri hilo
limeshakamilika uchunguzi wake na limefikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka ili
kuomba kibali cha kuwafikisha mahakamani watuhumiwa waliohusika na vitendo
hivyo vya rushwa.
Kwa mujibu wa ripoti ya awali kuhusu uchunguzi wa
mchakato wa ununuzi wa mabehewa mabovu uliofanywa na TRL, umebaini kuwa
menejimenti ya kampuni hiyo haikuwa makini kushughulikia maombi ya kuongezewa
muda, yaliyowasilishwa na Kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries
Limited.Uchunguzi ulibaini kuwa, mkataba wa zabuni namba PA/113/2012-13/ME/G/OE/014 ya ununuzi wa mabehewa 274, ya mizigo, Kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries Limited, iliwasilisha maombi ya kuongezewa muda Juni 13, 2014 na kurudia tena ombi hilo Septemba 12, 2014, lakini menejimenti ya TRL ilidaiwa kupuuza kwa kutojibu maombi hayo.
Zabuni nyingine inayochunguzwa ni namba PA/113/2012-13/ME/G/OE/013 iliyosainiwa kati ya TRL na kampuni hiyo Machi 21, 2013, inayohusu ununuzi wa mabehewa 25 ya mizigo yenye thamani ya Dola za Marekani 2,561,187.50.
Taarifa ya uchunguzi wa awali kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), inaeleza kwamba, zabuni hiyo iligawanywa katika makundi matatu, ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mabehewa 174 ya mizigo, mabehewa 50 ya kusafirisha mafuta ya petroli na mengine 50 kwa ajili ya mizigo.
No comments:
Post a Comment