ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Benard Membe, amesema ataendelea kumuunga mkono Rais Dk. John
Magufuli, kuzuia safari za nje ya nchi zisizokuwa na tija kwa taifa.
Pia, ameeleza kukerwa na baadhi ya vyombo vya habari na
mitandao ya kijamii, kuandika habari za upotoshaji, zenye lengo la
kumgombanisha na Rais Dk.Magufuli pamoja na kutaka kuisambaratisha CCM.
Amesema vyombo hivyo vya habari (sio Uhuru)na mitandao
ya kijamii, vimekuwa kwenye mkakati wa kutaka kuwagombanisha viongozi wastaafu
na serikali iliyoko madarakani, ikiwa ni mkakati wa vyama vya upinzani kutaka
kuivuruga CCM.
Hivyo, ametoa tahadhari kwa wanachama wa CCM kuwa makini,
hususan katika kipindi hiki, ambacho serikali ya awamu ya tano inaendelea na
jitihada za kupambana na ufisadi, kwa kutokubali kuchonganishwa.
Kauli hiyo ya Membe imekuja siku chache baada ya baadhi
ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kuandika habari zenye kumuhusisha
akipinga zuio la Rais Dk. Magufuli, la kufuta safari za nje zisizokuwa na
manufaa kwa taifa.
Akizungumza kwenye mahojiano maalumu, ambayo pia
yalirushwa na kituo cha televisheni cha Star, Membe alisema baadhi ya
wanahabari, ambao ni wapinzani wa CCM, wamekuwa wakipotosha kwa makusudi
ushauri unaotolewa na wanachama wa CCM kwa serikali.
“Yaani wanachukua sentensi moja halafu wanaipindua kwa
manufaa yao ya kisiasa huku wanaofanya vitendo hivyo, wanajulikana fika kuwa ni
maadui wa CCM,” alisisitiza kiongozi huyo wa zamani wa serikali ya awamu ya
nne.
Alibainisha kuwa, bado kuna hila zinazofanywa na vyama
vya upinzani, zinatokana na athari za kushindwa uchaguzi mkuu kwa sababu
ushindi wa CCM, unatokana na umoja wa wanachama wake.
“Tusikubali kuchonganishwa wala kufarakanishwa na wanafiki
wanaojulikana.Tulijua walikuwa wanapinga kushughulikiwa kwa ufisadi wao katika
kipindi cha uchaguzi,” alisema.
Membe aliongeza kuwa inapotekea baadhi ya watu
wanaondoka kwenye Chama, lazima CCM ifahamu kuwa kama kule walikokwenda
hawakufanikiwa, lazima watapanga mikakati ya kukisambaratisha.
Alisema ukifuatilia kwenye mitandao na vyombo vya habari,
kuna watu walikuwa vinara wa kupinga kuingia madarakani kwa Rais Dk. Magufuli
na kushughulikiwa kwa mafisadi.
Alisema kwa sasa kwenye mitandao hiyo, watu hao
wanajifanya vinara wa kuwashutumu watu waliokuwa mstari wa mbele kuhakikisha
CCM inaingia madarakani.
“Kuna watu wananishangaza kwani walikuwa vinara wa kupinga
kuingia madarakani kwa Rais Dk. Magufuli na walishiriki kukihujumu Chama ndani
na nje katika kipindi cha uchaguzi.
“Naamini bado kuna mabaki ndani ya CCM ambayo yanapaswa
kushughulikiwa,” alisisitiza.
Alisema ushauri alioutoa kwa serikali ni kuendelea
kuzuia safari za nje kwa viongozi, ambao hawana umuhimu wa kusafiri.
Hata hivyo alisema, iwapo itatokea mikutano ambayo rais
au waziri anapaswa kuhudhuria, watapaswa kusafiri.
Aliongeza kuwa Tanzania ina uhusiano na mataifa pamoja na
taasisi mbalimbali za kimataifa, hivyo kuna baadhi ya mikutano ambayo balozi
hatoweza kushiriki na atahijika rais au waziri kuhudhuria.
WALIOKIMBIA
CCM
Membe, ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la Mtama mkoani
Lindi, alisema CCM isiruhusu makapi yaliyokimbia kwenda kujiunga na vyama vya
upinzani, kurejea CCM.
Alisema endapo wakirejea CCM, matatizo yaliyopo ndani ya
Chama yatabaki palepale.
Akitoa mfano, alisema chama cha ANC cha Afrika Kusini,
kiliweka katazo kwa wanachama waliokihama kurejea ndani ya chama hicho.
Alisema kutokana na wanachama hao kuhama huku wakikidha,
Halmashauri Kuu iliweka maazimio ya kuzuia kutorejea tena.
“ANC iliweka maazimio na onyo kwa wale wote waliohama
huku wakikitukana, kukihadaa na kikidharau, licha ya kulelewa na kufundishwa
siasa na chama hicho, watashughulikiwa,” alieleza.
Alisema utaratibu huo umeweza kuwafunga midomo wanachama
wa ANC wanaokihama chama hicho kuacha kashfa na kukidharau.
No comments:
Post a Comment