Thursday, 28 January 2016

MBUNGE AHOJI LOWASSA, SUMAYE KULIPWA POSHO






UKUMBI wa Bunge jana, ulizizima wakati Hafidh Ali Tahir (Dimani-CCM), aliposimama na kuhoji ni kwanini serikali inaendelea kuwalipa posho na stahiki zingine mawaziri wakuu waliokimbilia vyama vya upinzani kusaka madaraka.
Amesema hakuna sababu kwa serikali kuendelea kuwalipa viongozi hao, ambao waliaminiwa na kupewa nafasi hiyo, lakini baadaye wamekimbilia upinzani kusaka vyeo.
Tahir alisema hatua ya serikali kuendelea kuwapa stahiki zinazotokana na jasho la wanyonge ni kuwakejeli Watanzania, hivyo ni muhimu sheria ikafanyiwa marekebisho haraka.
Kauli hiyo ya Tahir iliwaamsha kwenye viti Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na James Mbatia, kumkabili mbunge huyo huku wakimtuhumu kuuliza maswali ya uchochezi.
Katika swali lake la msingi, Tahir alihoji sababu za mawaziri hao bila kuwataja jina, kuhama CCM na kwenda upinzani huku wakiendelea kulipwa posho.
Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye na Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, waiikihama CCM na kukimbilia upinzani.
Lowassa, ambaye awali alikaririwa akisema atakuwa mwanachama wa mwisho kuhama CCM, alikimbilia CHADEMA kwa ajili ya kusaka nafasi ya kuwania urais, ambako hata hivyo alishindwa vibaya na mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli.
“Serikali haioni kuwa umefika wakati sasa wa kufanyia marekebisho sheria husika ili kufuta stahiki za mawaziri wakuu wastaafu wanaohama vyama vyao? Stahili zao zilitokana na nguvu za chama alichohama, hivyo kuendelea kumlipa ni sawa na kuwakejeli na kuwadharau wananchi waliomchagua,” alisema Tahir.
Mbunge huyo alikwenda mbali zaidi pale aliposema kuwa waziri mkuu huyo, baadaye anagombea urais na kushindwa, akisema kuwa ni ulafi wa madaraka.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angela Kairuki, alisema kujiunga na chama chochote au kujihusisha na masuala ya kisiasa ni haki ya kikatiba, ambazo haziwezi kuzuiwa wala kuingiliwa.
Alisema mawaziri wakuu wastaafu wanahudumiwa kwa mujibu wa sheria ya mafao kwa hitimisho la kazi viongozi, namba 3 ya mwaka 1999.
Angela alisema sheria haielezi hatua zinazopaswa kuchukuliwa kwa waziri mkuu mstaafu, atakayeamua kuhamia chama kingine cha siasa tofauti na kilichomweka madarakani na kumwezesha kushika wadhifa huo.
“Licha ya sheria hiyo kutoweka zuio lolote kwa viongozi wa kitaifa wastaafu kujiunga na chama kingine cha siasa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inalinda haki za msingi za binadamu, ikiwemo haki ya uhuru wa mtu kujihusisha na masuala ya kisiasa,” alisema.
Angela alisema ibara ya 20 (1) ya Katiba, inasema mtu yeyote ana haki ya kujihusisha na mambo ya kisiasa.
“Mawaziri wakuu wastaafu kama walivyo watu wengine, wanao uhuru wa kujiunga na chama chochote cha kisiasa wanachokipenda ili mradi hawavunji sheria,” alisema.
Alisema suala la kufanyia marekebisho sheria ya mafao kwa viongozi wa kitaifa wastaafu, namba 3 ya mwaka 1999, kwa lengo la kuwazuia mawaziri wakuu wastaafu au viongozi wengine wa kitaifa wastaafu kujiunga na chama chochote cha kisiasa, linakwenda kinyume na Katiba.
Kwa upande wake, Mbowe alidai  Tahir hajui Katiba na kumtuhumu kuwa ni mchochezi na kueleza kuwa kumekuwepo na tatizo la kushindwa kutofautisha majukumu ya CCM na serikali.
Aidha, Mbatia katika kumjibu Tahir, alisema kwa kuwa wabunge majukumu yao ni kuwa na uelewa mkubwa, waziri haoni umuhimu wa kutoa semina kwa wabunge ili wapate uelewa wa kutumia muda wao kwa maslahi ya taifa.
Hata hivyo, Angela alisema swali la Tahir si la uchochezi na kwamba, ndiyo sababu amelijibu na upande wa upinzani umeyafurahia majibu yake.
Naye, Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini-CCM), katika swali lake la nyongeza, alihoji sababu za kutofanyiwa marekebisho kwa sheria hiyo ili pensheni itolewe pale mtu atakapokuwa amekwenda kutulia baada ya kustaafu na si kuhangaika kuhemea kwingine.
Katika majibu yake, Angela alisema stahili hizo pamoja na pensheni ya mwaka zinatolewa kwa mujibu wa sheria namba 3 ya 1999.
Alisema masharti yaliyopo kwa wastaafu hao ni kutotakiwa kutoa siri kuhusiana na masuala mbalimbali waliyotumikia wakiwa madarakani.

No comments:

Post a Comment