UKUMBI wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano jana uligeuka kuwa uwanja wa mapambano baada ya wabunge wa
kambi ya upinzani kuondolewa ndani ya ukumbi na askari wa bunge, wakisaidiana
na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasi (FFU).
Hali hiyo
ilijitokeza baada ya wabunge hao kupinga kuendelea kwa kikao cha Bunge
cha kujadili hotuba ya Rais John Magufuli, badala yake wajadili hatua ya
serikali ya kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya Kituo cha Televisheni ya
Taifa (TBC).
Vurugu hizo zilizuka
baada ya kipindi cha mchana kuanza, ambapo Mwenyekiti wa Bunge, Andrew
Chenge, alisimama na kutoa maamuzi ya Kamati ya Uongozi, iliyokutana jana,
asubuhi, baada ya taarifa ya serikali juu ya hatua hiyo.
Baada ya Chenge kusimama,
alisema kamati imeamua kuwa bunge liendelee kujadili hotuba ya Rais.
Alisema kamati
hiyo pia imetoa uamuzi mbunge husika, ambaye alitoa hoja ya kutaka kuahirishwa
kama hajaridhika, anaweza kukata rufaa kwa utaratibu uliopo.
“Kamati ya
uongozi imeamua kuwa mjadala uendelee kama ilivyopangwa na kama mbunge yeyote
hajaridhika, anaruhusiwa kuwasilisha malalamiko yake kwa katibu wa Bunge,”
alisema Chenge.
Mara baada ya mwenyekiti
kusoma taarifa hiyo, aliwataka wabunge kuendelea na mjadala, ndipo Mbunge
wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, aliposimama na kuomba mwongozo wa Spika.
Katika muongozo
wake, Lissu alitaka kujua kama Kamati ya Uongozi ina mamlaka ya kutoa maamuzi
yanayohusu bunge.
Baada ya kupewa
mwongozo, wabunge wengine Ester Bulaya na John Heche, walisimama na kutaka
kuomba mwongozo, ndipo mwenyekiti alipokataa kuendelea na miongozo.
Hata baada ya
kukataa kutolewa kwa miongozo hiyo, Lissu aliendelea kusimama huku akiwataka
wabunge wote wa kambi ya upinzani kusimama.
Chenge
aliendelea kuwasihi wabunge hao kukaa chini, lakini bila mafanikio huku wakitoa
maneno ya kejeli dhidi ya kiti.
Ndipo Chenge alipotoa
amri ya kuwataka wabunge hao kutoka kama wanaona hoja hiyo ya kujadiri hotuba
ya rais haina mashiko kwao.
“Nimeshasimama
mara nne kuwasihi, sasa naona mnataka kukulifanya bunge kutofanya shughuli zake
zilizopangwa leo, hivyo nawaomba mtoke nje,” alisema.
Baada ya kauli
hiyo, ndipo mwenyekiti huyo alipowataja wabunge wanne, ambao ni Tundu Lissu,
Ester Bulaya, Godbless Lema na Pauline Gekul kuwa watoke nje ya ukumbi.
Kauli hiyo ya
mwenyekiti ilimfanya Lema kuinuka na kutoa tai, huku akisema kuwa hatoki nje na
yupo tayari kuuawa ndani ya ukumbi wa bunge.
Hapo ndipo vurugu
zilipoanza na kusababisha kuitwa askari wa bunge na baadaye askari wa FFU
waliingia ukumbini kuongeza nguvu.
Baada ya askari
hao kuingia bungeni, waliendelea kuwasihi wabunge hao watoke, lakini walikaidi
na kuendelea kupiga kelele.
Kutokana na
wabunge hao kukaidi amri hiyo, askari hao walianza kuwatoa kwa nguvu mmoja
mmoja huku wengine wakigoma kutoka na kubebwa juu juu hadi nje.
Kiongozi wa
upinzani bungeni, Mbowe alipoona kazi ya kuwatoa bungeni wabunge hao
ikifanyika, aliamua kutoka kwa hiari huku akisindikizwa na polisi.
Katika lango kuu
la kuingilia ukumbi wa bunge, kulikuwa na idadi kubwa ya polisi, wakiwa na mbwa
kwa ajili ya kuimarisha ulinzi.
Wakati vurugu
zikiendelea ndani ya ukumbi, wabunge wa CCM walionekana kuwa wapole na walikaa
kwa utulivu wakiwashangaa wenzao.
Awali, akitoa
kauli ya serikali kuhusu Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alisema shirika hilo lilianza
kurusha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge mwaka 2005.
Nape alisema
kabla ya TBC kuanza kurusha matangazo hayo moja kwa moja, wakati huo ikijulikana
kama Televisheni ya Taifa (TVT), ilikuwa inarekodi matukio yote ya bunge na
kurusha usiku katika vipindi maalumu, vilivyofahamika kama ‘Bungeni Leo’ kwa
maana ya yaliyojiri ndani ya ukumbi wa bunge kwa siku husika.
Alisema baada ya
kuanza kwa utaratibu wa kurusha matangazo moja kwa moja mwaka 2005, gharama za
kufanyakazi hiyo zimekuwa zikipanda kwa kasi hadi kufikia sh. bilioni 4.2, kwa
mwaka kwa mikutano minne.
Nape alisema
shirika lilikuwa likigharamia kwa sehemu kubwa matangazo hayo kwa kutumia
mapato yake yanayotokana na matangazo madogo ya biashara.
“Ifahamike kuwa
asilimia 75, ni vipindi vinavyolenga kutoa elimu kwa umma na asilimia 25 ni
burudani,” alisema.
Alisema kutokana
na hali hiyo, TBC imeona ni busara kubadilisha mfumo wa utangazaji wa shughuli
za bunge ili kukabiliana na kuzidi kupanda kwa gharama za uendeshaji.
“TBC imeona ni
busara kuanzia mkutano huu wa bunge, iwe inarusha baadhi ya matangazo ya moja
kwa moja, ikiwa ni njia ya kubana matumizi,” alisema.
Alisema chini ya
utaratibu huo, shirika litahakikisha kuwa baadhi ya matukio ya bunge,
yatarushwa moja kwa moja na mengine kurekodiwa na kuandaliwa kipindi maalumu,
kitakachoitwa ‘Leo Katika Bunge’.
Waziri huyo
alisema kipindi hicho kitakuwa na mambo yote muhimu yaliyojiri ndani ya bunge
kwa siku husika.
Alisema kipindi
hicho kinarushwa kuanzia saa 4:00 usiku, hadi saa 5:00 usiku, kilianza jana na
tayari baadhi ya wananchi wameonyesha kuridhishwa na utaratibu huo.
Nape alisema
uamuzi huo utapunguza gharama za uendeshaji kwa shirika na pia kwa kupitia
kipindi cha Leo Katika Bunge, Watanzania wengi watapata nafasi ya kufahamu
yaliyojiri bungeni.
Alisema wakati
mijadala ya bunge ikiendelea Watanzania waliowengi wanakuwa na kazi za kiofisi au zingine za
ujenzi wa taifa kwa mahali walipo.
Baada ya kutoa
taarifa hiyo, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, alisimama na
kuomba mwongozo kwa Mwenyekiti, kuwa muda uliopita Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, alitoa kauli kuwa TBC haitarusha matangazo ya bunge ya moja
kwa moja kama ilivyozoeleka.
Alisema TBC ni
televisheni ya taifa, sio ya biashara, lakini inafanya biashara kwa sababu serikali
imeinyima mafungu, lakini hotuba ya rais alipolihutubia bunge ilionyeshwa moja
kwa moja.
Zitto alihoji wa
nini wabunge wanapoijadili hawatakiwi
kuonyeshwa na kwamba, kufanya hivyo ni kuwanyima haki wananchi.
Akijibu hoja
hiyo, Chenge alisema: “Nimesikia Zitto kauli yake, ambayo msingi wake ni kanuni
ya 49. Uamuzi wangu, kama Zitto anaona upo umuhimu wa hoja hiyo, lete kwa
utaratibu unaofuata, hivyo naomba shughuli ziendelee.”
Wakati hayo
yakiendelea, wabunge wote wa upinzani walisimama huku wakiomba mwongozo, ambapo
licha ya mwenyekiti kusimama, nao waliendelea kusimama.
Kutokana na hali
ilivyokuwa inaendelea ndani ya ukumbi wa bunge, baadhi ya askari wa bunge
waliingia ukumbini na kukaa karibu na meza ya mwenyekiti.
Licha ya askari
hao kuingia bungeni, wabunge hao wa upinzani waliendelea kusimama na kuzungumza
bila kufuata utaratibu.
Kufuatia zogo
hilo, Chenge alisema suala hilo litafikishwa kwa kamati ya uongozi na
kusitisha shughuli za bunge kwa saa moja.
Baada ya kusitisha
shughuli hizo, wabunge hao wa upinzani walisikika wakisema ‘Chenge, Chenge,
Chenge, Mtemi, Mtemi’.
Akitoa maoni
yake, Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia, alisema serikali imefanya vyema
kukatisha matangazo ya moja kwa moja kwani wabunge wengi wamekuwa wakitumia
mwanya huo kujipatia umaarufu na kutafuta sifa.
Mbunge wa Mlalo
(CCM), Rashid Shangazi, alisema Chenge alifanya jambo la maana kwa kuheshimu
kanuni na kutoa nafasi kwa kamati ya uongozi kujadili suala la kukataza kurusha
matangazo lijadiliwe na kupatiwa ufumbuzi.
Mbunge wa Tarime
Vijijini (Chadema), John Heche, alisema serikali kuondoa matangazo hayo, inasikitisha
kwa madai kuwa nchi inaingia katika zama za udikteta.
No comments:
Post a Comment