Tuesday, 5 January 2016

KIAMA CHA WAHAMIAJI HARAMU CHAJA




SERIKALI imetangaza vita na wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha sheria kwa kuiagiza Idara ya Uhamiaji, kuwasaka popote waliko na kuwachukulia hatua za kisheria, ikiwemo kuwarudisha makwao.

Pia, imetoa ruhusa kwa idara hiyo kumnyima kibali cha kuishi nchini, mtu wanayemtilia shaka, lakini ana vielelezo vingine vya kumruhusu kuishi, ikiwemo hati ya biashara na leseni kwa kigezo kuwa idara hiyo ina mamlaka ya kufanya hivyo.

Imesema hakuna namna nyingine kwa kuwa tatizo la uhamiaji haramu limekuwa kubwa na linaendelea kukua kadri siku zinavyokwenda, hivyo wakati umefika wa kupambana nalo kila kona ya nchi ili kuhakikisha linatoweka na wahusika wanadhibitiwa.

Agizo hilo lilitolewa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Masauni Hamad Masauni, kwa wakuu wa idara mbalimbali za Uhamiaji na makamishna, alipozungumza nao baada ya kuhitimisha ziara yake ya saa nne, makao makuu ya Uhamiaji, Kurasini.

Masauni alisema serikali ya awamu ya tano ina nia ya dhati ya kutatua changamoto zinazoikabili Idara ya Uhamiaji ili itekeleze majukumu yake kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu, kwa kuwa uwepo wa wahamiaji haramu ndani ya nchi una madhara makubwa kuliko inavyodhaniwa.

“Wahamiaji wasio na tija kwa maendeleo ya nchi hatuna budi kuwaondosha, hakikisheni mnawatafuta kwa kutumia misako ya kisayansi kila kona ya nchi kisha muwaondoe. Haiwezekani mhamiaji akaja kwetu kufanyakazi ambayo Mtanzania anaiweza.

“Yapo madhara mengi yanayotokana na uhamiaji haramu, kubwa ni uhalifu, halafu yanafuata mengine kama ukosefu wa ajira kwa wazalendo, kibaya zaidi wahamiaji hawa ndio wa kwanza kuvunja sheria za nchi, hasa kukwepa kodi,” alisema Naibu Waziri.

Alitoa rai kwa watumishi wa Uhamiaji kutekeleza maelekezo ya serikali na kutoa mrejesho wizarani kila baada ya wiki, ambapo alisema ili kufanikisha hilo, hawana budi kukiimarisha kitengo cha ukaguzi, ambacho kimekuwa kikilalamikiwa kwa muda mrefu.

Alisema kipindi cha nyuma kulikuwa na vibali vya muda, ambavyo vingesaidia utekelezaji majukumu ya idara, lakini serikali ilivisitisha kutokana na kukumbwa na changamoto ya matumizi mabaya.

“Vibali vya muda serikali ilivisimamisha, vilikuwa na mchango mzuri kwenye utekelezaji wa majukumu ya idara, lakini ndio hivyo, watu walivitumia vibaya, sasa serikali inahitaji maelezo ya sababu za kukwama vibali vile ili zitatuliwe, vianze tena kama itawezekana.

“Kwa watakaobainika kushiriki kwenye kuua mfumo ule, itabidi watupishe, waondoke kwa sababu wako watu wengi mitaani hawana kazi na wanaitafuta kweli kweli, lakini kwa sasa fanyeni kazi kufikia malengo mliyojiwekea,” alisema.

Aidha, Masauni alisema ziara yake katika idaya hiyo ni ya kwanza tangu kuteuliwa na Rais Dk. John Magufuli, kuwa msaidizi wa Waziri Charles Kitwanga, kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani, ambapo malengo yake ni kuona idara hiyo na zingine chini ya wizara yake zinafanyakazi kwa ufanisi mkubwa.

Alisema hadi kufikia sasa, yapo mengi mazuri yaliyofanywa na Uhamiaji, lakini pia changamoto zinazoikabili ni lazima serikali izisimamie na kuzitatua kadri itakavyowezekana kwa kuwa idara hiyo ni muhimu kwa usalama wa nchi.

Awali, akisoma risala kwa Naibu Waziri Masauni, Kamishna wa Uhamiaji (Utawala na Fedha), Piniel Mgonja, alisema idara hiyo inajitahidi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, lakini wanaandamwa na changamoto lukuki zinazokuwa kizuizi kwenye utekelezaji wa majukumu yao.

Alizitaja changamoto hizo kuwa ni uhaba mkubwa wa rasilimali watu, ambapo kuna jumla ya watumishi 2,770, huku hitaji likiwa ni watumishi 8,616, ufinyu wa bajeti kutoka hazina, uhaba wa nyumba 2,442 za watumishi na uhaba wa ofisi 89.

Alisema pamoja na changamoto hizo, wanaiomba serikali itenge maeneo maalumu kwa kujenga vituo vya kutunzia wahalifu wa uhamiaji, badala ya kutegemea mahabusu na magereza ambazo zina changamoto ya mlundikano.

Sambamba na hilo, alisema kwa kipindi cha miaka minne kuanzia Januari 2011, wamefanikiwa kutoa hati za kusafiria kwa Watanzania 333,219, vibali vya muda vya kuishi kwa raia wa kigeni 67,560, ambao kati ya hao 561, walipewa uraia.

Aidha, alisema kutokana na misako iliyofanyika kote nchini, walifanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 50,958 na kuwachukulia hatua mbalimbali za kisheria.

Ziara hiyo ya naibu waziri inafuatia ziara ya Waziri Kitwanga, aliyetembelea idara hiyo Oktoba 22, mwaka jana na kuagiza kufanyika operesheni kabambe ya kuwasaka wahamiaji hao kuanzia juzi.

No comments:

Post a Comment