NA MWANDISHI WETU
WAZIRI wa Katiba na
Sheria, Dk. Harison Mwakyembe, amesema sekta ya sheria imegubikwa na majipu
sugu yanayohitaji kupasuka yenyewe kabla Rais Dk. John Magufuli hajayatumbua kwa
uchungu.
Ametahadharisha kuwa majipu
makubwa na vijipu uchungu, visisubiri kutumbuliwa bila ganzi kwa kuwa hayuko
tayari kuonekana mzembe kwa kucheka na wala rushwa, wanaoathiri utendaji kazi
wa serikali katika kutoa haki kwa wananchi.
Aidha, Dk. Mwakyembe amesema
mchakato wa kuundwa kwa mahakama ya mafisadi, ulioahidiwa na Rais Magufuli wakati
wa kampeni, bado upo pale pale kwa kuwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Waziri huyo wa katiba na
sheria, pia ameahidi kumuunga mkono kikamilifu Dk. Magufuli katika kukamilisha
mchakato wa Katiba Mpya ili Tanzania iwe na katiba bora yenye kukidhi mahitaji
ya wananchi
Dk. Mwakyembe alisema
hayo jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kukutana kwa
zaidi ya saa tatu na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga pamoja na
vigogo wengine wa sekta hiyo.
Katika kikao hicho
kilichofanyika ofisini kwa DPP, mjini Dar es Salaam, Dk, Mwakyembe na Mganga,
walijadili kwa kina kuhusu mikakati ya utendaji kazi mpya wenye tija katika
serikali ya awamu ya tano.
Dk. Mwakyembe
alisema utendaji haki unagusa maisha ya
wananchi, hivyo ubora wa huduma ni muhimu.
“Utendaji kazi wenu sasa
uwe karibu na wananchi kwa kuwa hakuna siri, makarani, washauri, mahakimu,
wasimamizi wa magereza ni tatizo, hivyo mjitambue kuwa ni sehemu ya serikali,
mkitetereka mnatutia dosari na kwa sasa mko rehani,”alisema.
Alisema utoaji huduma wa
haki kwa wanasheria, polisi, majaji una vijipu uchungu, ambavyo havivumiliki na
kamwe hawezi kuwavumilia, hivyo kabla Rais Dk. Magufuli hajavitupia jicho na
kuvitumbua bila ganzi, atahakikisha amevisafisha vya kutosha.
“Rushwa ni jipu kubwa
linaloudhi serikalini na wananchi wanajua toka uhuru na tangu uongozi wa Mwalimu
Julius Nyerere, kuwa jipu hili ni adui wa haki. Uzuri mimi waziri wenu pia ni
mwanasheria na wengi wenu ni wanafunzi wangu, hapa tuache kujipa matumaini,
sasa ni kazi tu na kila mtu ajisafishe leo, asingoje kesho maana
ameshachelewa,”alisema.
Aliongeza: “Wanasheria
tunajijua, ni mafundi wa kujiliwaza kwa kuwa tunajidanganya na vifungu vya
sheria. Sasa mtambue kampeni ya serikali ya awamu ya tano ni kusafisha uchafu
serikalini na rais wetu amejitoa mhanga kubadili nchi,”alisema.
Aliwataka watendaji wa
sekta hiyo kutambua kuwa atakayechukuliwa hatua, asitarajie wananchi watampa
nafasi ya kujitetea kwa kuwa wamechoshwa na vyombo vinavyotoa haki kuwa sehemu
ya ubadhirifu.
Alisema hakuna vyombo
vya serikali vinavyoweza kubadili mfumo wa uozo kama vyombo vya sheria kwa
kuzingatia maadili katika uandaaji mashitaka na hukumu.
Dk. Mwakyembe alisema
anaelewa mazingira magumu ya kazi za mawakili wa serikali, kwa kuwa mawakili
binafsi wana malipo makubwa, hivyo wakati serikali inajipanga kuiwezesha sekta
hiyo, lazima kufumuliwa wachache walio
wachafu ili wakae pembeni.
“Watanzania wamechoka,
wanataka mabadiliko, mchezo wa kuchelewesha mafaili mahakamani kwa makusudi,
kubambikia watu kesi, sasa basi. Ubora wa huduma unaeleweka, hivyo badilikeni
haraka, wengi humu ni wachafu na mimi sipo tayari kusubiri hatua za Dk.
Magufuli,”alisema.
Alimuahidi DPP Mganga
kuijengea uwezo ofisi hiyo katika kukabiliana na kesi za dawa za kulevya kwa kuwa
ni changamoto kubwa kwa serikali.
Akizungumzia mchakato wa
Katiba Mpya, Dk. Mwakyembe aliwatoa hofu wananchi kwa kusema kuwa, Rais
Magufuli ndiye msemaji wa mwisho wa serikali na amelizungumzia jambo hilo mara
kwa mara, kwamba ni kiporo alichoachiwa katika serikali awamu ya nne.
Alisema kutokana na
ahadi za Dk Magufuli katika kufanyiakazi mchakato wa katiba mpya, atahakikisha
anamuunga mkono kikamilifu ili Tanzania iwe na katiba bora yenye kukidhi
mahitaji ya wananchi.
Pia, alisema mchakato wa
kuundwa kwa mahakama ya mafisadi upo pale pale na muda mfupi ujao majibu
yatapatikana.
“Mahakama ya mafisadi ni
suala lililo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM na imebaki utekelezaji, muda mfupi
ujao majibu yatapatikana,”alisema.
No comments:
Post a Comment