Monday, 1 May 2017

JPM: NITAENDELEA KUWATUMBUA WATUMISHI WASIO NA WELEDI


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, amesema ataendelea kuwatumbua watumishi wa umma wanaokiuka maadili na pia kuwa mkali katika kusimamia nidhamu ya fedha za umma.

Amesema hawezi kuvumilia kuona fedha za umma zikiendelea kutafunwa na watu wachache kwa kujipa mishahara hewa na safari za nje, ambazo hazina tija kwa wananchi.

Ameongeza kuwa, nchi ilikuwa imejaa mianya ya rushwa, hali iliyokuwa ikiwaumiza wananchi wa kipato cha chini na kuahidi hatafumbia macho kuona wananchi wakinyanyasika.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana, katika misa ya Jumapili, iliyofanyika kwenye Katika Kuu la Kiaskofu la Kristu Mfalme, Jimbo Katoliki Moshi na baadaye kushiri ibada katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, yaliyoko Moshi mkoani Kilimanjaro.

Alisema maamuzi na hatua zinazochukuliwa na serikali ya awamu ya tano, yanalenga kuleta maendeleo kwa Watanzania na sio vinginevyo, kama ambavyo amekuwa akinukuliwa na baadhi ya watu kuwa ni mtu katili.

“Serikali ya awamu ya tano imejidhatiti katika kuhakikisha kuwa inawaletea maendeleo wananchi bila kujali itikadi ya vyama vyao, hivyo hakuna haja ya baadhi ya watu au mtu kunitafsiri vinginevyo, kwani serikali ilikuwa imejaa madudu mengi,” alisema Dk. Magufuli.

Aliongeza: “Baba Askofu, hatua ambazo ninazichukua za kutumbua majipu watumishi wasio na weledi, lazima zifikie katika kuwaletea maendeleo Watanzania wote. Kulikuwa na maovu makubwa ndani ya serikali, kulikuwa na watumishi hewa 19,000 na hawa wanalipwa mishahara hewa, jambo hili haliwezi kufikia malengo ambayo tumejiwekea."

Rais Magufuli alisema baada ya kuchaguliwa kuwa rais, watu walichokuwa wanatarajia kukiona ni maendeleo wanayotaka, ambapo alirudia kauli yake kwa Watanzania pale aliposema hatawaangusha.

Huku akishangiiiwa na waumini waliohudhuria ibada hiyo, Rais Magufuli aliyapongeza madhehebu ya dini kwa ushirikiano yanayaotoa kwa serikali katika kuchangia shughuli za maendeleo katika nyanja mbalimbali.

Alifafanua kwamba, serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu yote katika kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo huku akiwataka kila mmoja kufanyakazi kwa bidii.

Awali, katika mahubiri yake, Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi, Mhashamu Isaac Amani, alisema Watanzania hawana budi kuwaenzi waasisi wa Taifa la Tanzania kwa kufanyakazi.

“Mwalimu Julius Nyerere na wenzake walifanya kazi kubwa katika kuleta Uhuru wa nchi hii, hivyo na sisi tusifurahie Uhuru wetu kwa kukaa tu, badala yake tufanyekazi na kuleta maendeleo”, alisema.

Aliongeza: “Uhuru tulioupata ni sawa na shamba lililolimwa, ambalo ni lazima listawishwe ili liweze kutoa mazao mazuri na yenye manufaa.”

Katika ibada hiyo, Rais Magufuli alitoa mchango wa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya shughuli ya ujenzi unaoendelea katika parokia ya Kristu Mfalme, pamoja na shilingi milioni moja taslimu kwa ajili ya maendeleo ya Utume wa Kwaya.

Akiwa katika Ibada ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Usharika wa Moshi Mjini, Rais Magufuli pia alitoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya shughuli ya ujenzi kanisani hapo.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Fredrick Shoo, alisema wapo baadhi ya watu hawana amani, utulivu kutokana na uchafu, ambao wamekuwa wakiufanya, hivyo kuwa na hofu ya Mungu.

Aidha, Askofu Dk. Shoo alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa ya kutumbua majipu ndani ya serikali na kutokatishwa tamaa na baadhi ya watumishi, ambao ni wachafu.

No comments:

Post a Comment