BAADHI ya wasomi na wanasiasa nchini wamepongeza
juhudi za serikali za kuwaondoa watumishi walioghushi vyeti huku wakiomba
ukaguzi huo usiishie sarikalini tu bali uguse hata taasisi nyingine.
Kauli za wasomi na wanasiasa hao zimekuja siku
chache baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Angellah Kairuki, kuweka hadharani majina ya watumishi walioghushi vyeti.
Baada ya kupokea ripoti hiyo kutoka kwa Waziri
Kairuki, Rais, Dk. John Magufuli aliamua kuwafuta kazi watumishi wote 9,932
waliobainika kughushi vyeti.
Pia, aliagiza ifikapo Juni 15, mwaka huu, watumishi
hao wafikishwe mahakamani endapo wataikaidi kujiondoa wenyewe.
Aidha, alisisitiza kuwa majina ya watumishi hao
yachapishwe gazetini ili kila mmoja awafahamu.
Aliongeza kuwa, watumishi wengine 1,538, ambao
vyeti vyao vina utata kwa kutumiwa na watumishi zaidi ya mmoja, wachunguzwe kwa
kina ili kujua ni nani mhusika, ambaye anastahili kupata mshahara.
Wakizungumza na Uhuru kwa nyakati tofauti mjini Dar
es Salaam, jana, wasomi hao walisema juhudi zinazofanywa na serikali,
zinatakiwa kupongezwa kwa sababu haiwezekani watu wasio na vyeti wafanyekazi na
wenye vyeti wahangaike mitaani.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa
Benson Banna, alisema watumishi hao wamefukuzwa kazi, lakini kila mmoja
anatakiwa kujiuliza wameingiaje serikalini.
“Lakini ni lazima twende mbali, waliingiaje ingiaje
pale na hadi kuajiriwa? Na mamlaka za kudhibiti vyeti na kuvihakiki walikuwa
wapi?” Alihoji.
Alisema inatia ukakasi kuona menejimenti ya
rasimaliwatu haifanyikazi zake vizuri hadi kuruhusu watumishi kufanyakazi
wakiwa na vyeti vya kughushi.
“Mifumo katika menejimenti ya rasilimali watu
inatakiwa kusimamia suala hili vizuri ili dosari iliyojitokeza isiweze kutokea tena,” alisema.
Pia, alishauri wale wote waliofukuzwa kazi, wapewe
stahiki zao ili waweze kujikimu wanapokwenda kuanza maisha mapya.
Hata hivyo, alisema zoezi hilo lisiishie serikalini
tu, bali linatakiwa kufika kwa wanasiasa, mawaziri, wabunge, wenyeviti wa
mitaa, vijiji na watendaji.
Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Dk.
Thimothy Lyanga, alisema mtu aliyeghushi cheti halafu akaenda kufanyakazi, siku
zote anakuwa hana maadili ya kazi.
“Kama
umeweza kughushi cheti, hata ukienda kufanyakazi ni lazima utakuwa hauna
maadili. Na hawa watu ndiyo wanaofanya kunakuwa na rushwa, maana maisha yao
yanazungukwa na udanganyifu,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, aliishauri serikali kufanya
zoezi hilo kuwa endelevu ili waweze kuwatambua wale wote, ambao wanaghushi
vyeti na kusababisha wenye vyeti halisi kukosa kazi.
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe,
naye ameunga mkono uamuzi wa serikali wa kuwachukulia hatua watumishi wote wa
umma waliobainika kutumia vyeti feki, ikiwemo kuwafukuza kazi na kuwafikisha
kwenye vyombo vya sheria.
“Bila shaka hatua hii itapanda mbegu ya
uwajibikaji, kuchochea uadilifu na kuhakikisha weledi kwenye utumishi wa umma,”
alisema.
Aidha, alisema kauli ya Rais, Dk. John Maguli ya kuwasamehe wale watakaojiondosha kazini
wenyewe na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wale watakaoendelea kubaki
kwenye nafasi zao, ni kinyume cha sheria na katiba ya nchi.
“Kisheria Rais hana mamlaka ya kumsamehe mtu
anayetuhumiwa kufanya kosa la jinai iwapo mtu huyo hajafikishwa kwenye vyombo
vya sheria na kuhukumiwa,” alisema.
Pia, aliishauri serikali kufanya mchakato huo wa
vyeti ili uguse viongozi wa kisiasa wa vyama vya upinzani na CCM.
No comments:
Post a Comment