Wednesday, 13 July 2016

KUMEKUCHA CCM DODOMA, MAANDALIZI MKUTANO MKUU YAKAMILIKA





CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mkutano mkuu maalumu, utakaofanyika Julai 23, mwaka huu, mjini Dodoma, yamekamilika na kwamba hakuna mwenye uwezo wa kuuzuia.

Aidha, CCM kimesema ajenda pekee ya mkutano huo ni kumchagua mwenyekiti mpya wa Taifa, atakayechukua nafasi ya Mwenyekiti wa sasa na Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Kimesema jumla ya wajumbe 2,432 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, wanatarajiwa kuhudhuria mkutano huo na wanatakiwa wawe wameshafika Dodoma ifikapo Julai 22, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari wa Uhuru, ofisini kwake, mjini Dar es Salaam, jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Rajabu Luhwavi alisema mkutano huo utafanyika kwa mujibu wa Katiba ya Chama na unatambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Luhwavi alisema tishio la hivi karibuni lililotolewa na Baraza la Vijana la Chadema (BAVICHA) la kutaka kuzuia kufanyika kwa mkutano huo halina maana na haliwezi kuwaumiza vichwa na linapaswa kupuuzwa.

Alisema ingekuwa wanaotaka kuharibu mkutano huo wanatoka ndani ya CCM au kuna watu wasio wanachama wanataka kuhudhuria mkutano huo kwa nguvu, kungeweza kuwa na tatizo.

"Lakini huu ni mkutano wa kikatiba wa CCM na tumeshatoa taarifa kwa msajili. Ingekuwa tunafanya mkutano siku moja na chama kingine cha siasa, lingekuwa tatizo.

"CCM itafanya mkutano wake kwenye ukumbi wetu na watakaohudhuria ni wanachama wa CCM,"alisisitiza Luhwavi.

Luhwavi alisema mkutano huo upo kwenye kalenda ya Chama na umelenga kukiimarisha na kuthibitisha kwa vitendo jinsi demokrasia ilivyojengeka ndani ya CCM.

Alisema Chama kinatarajiwa kuandika historia nyingine mpya miongoni mwa vyama vya siasa kwamba, uongozi ni dhamana na demokrasia inatokana na maamuzi ya w atu.

Naibu Katibu Mkuu alisema ingewezekana kwa Mwenyekiti mstaafu, Kikwete na Mwenyekiti mpya mtarajiwa, Rais Dk. John Magufuli kupokezana uongozi kwa njia za kawaida, lakini kwa kuwa Chama kinaendeshwa kwa misingi ya Katiba, ndio sababu kimepanga kukutana mjini Dodoma.

Luhwavi alisema kukabidhiana madaraka kwa viongozi hao, kumetokana na utamaduni uliojengeka ndani ya CCM kwa mwenyekiti anayekuwepo madarakani kukabidhi madaraka kabla ya muda wake kumalizika.

"Uzoefu unaonyesha kuwa baada ya rais kuchaguliwa, rais anayekuwepo madarakani anaridhia kukabidhi madaraka mapema. Hivyo Kamati Kuu na Halmashauri Kuu zitapendekeza jina la mwanachama mwenye sifa ya kuwa mwenyekiti. Na anayependekezwa ni rais aliyeko madarakani,"alisisitiza.

Kwa mujibu wa Luhwavi, mkutano mkuu utatanguliwa na kikao cha Kamati Kuu kitakachofanyika Julai 20, mwaka huu na kufuatiwa na kikao cha Halmashauri Kuu kitakachofanyika Julai 22, mwaka huu.

Alisema baada ya mkutano mkuu kumalizika, mwenyekiti mpya ataitisha kikao cha Halmashauri Kuu kitakachofanyika Julai 24, mwaka huu, ambapo kitapokea na kuthibitisha mapendekezo ya mwenyekiti kuhusu nafasi za wajumbe wa sektretarieti.

Luhwavi alisema wajumbe watakaohudhuria mkutano huo kutoka mikoa ya Kusini, Nyanda za Juu, Kaskazini na Zanzibar watasafiri kwenda Dodoma kwa mabasi wakati wale wanaotoka mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Tabora, Simiyu na Geita watasafiri kwa treni.

Alisema wajumbe wote wameshaandaliwa mahali pa kulala na kusisitiza kuwa, kamati zote zimejipanga vyema kuhakikisha wajumbe hawapati usumbufu muda wote watakaokuwa Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu alisema wametoa mwaliko kwa vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu, kuhudhuria sherehe za ufunguzi wa mkutano mkuu, sambamba na mabalozi wa nchi za nje walioko nchini na viongozi wa vikundi mbalimbali vya kijamii, yakiwemo madhehebu ya dini.

Pia, alisema mkutano huo utahudhuriwa na viongozi mbalimbali wastaafu wa CCM, wakiwemo wenyeviti wa taifa na wake wa viongozi wastaafu, wakiwemo Mama Karume na Mama Maria Nyerere.

No comments:

Post a Comment