RAIS mstaafu wa awamu ya nne, Dk. Jakaya Kikwete amesema hajawahi kufikiria kuomba kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), lakini iwapo atapendekezwa hawezi kuacha kuitumikia.
Amesema amefanya kazi kubwa duniani katika kipindi cha uongozi wake, hivyo hatarajii kuandika barua ya kuomba kazi yoyote kwa sasa.
Dk. Kikwete alisema hayo mjini Dar es Salaam, jana, wakati wa mkutano wa kikanda wa sera za tabianchi.
Alisema anashangaa kutajwa kwamba amependekezwa kuwania nafasi hiyo huku akiwa hajaiomba.
Rais huyo mstaafu alisema anatambua mchango wake katika dunia ni mkubwa, hivyo haoni haja ya kuomba nafasi yoyote ya kazi, lakini iwapo Umoja wa Mataifa utaona anafaa kuwatumikia, atajitolea kwa nguvu zote.
“Kwanza sijaomba, nashangaa naambiwa mara nipo katika tatu bora, mara hivi, mara hivi, sijui hizo habari zinatoka wapi, lakini niseme tu kwamba, mchango wangu katika hii dunia ni mkubwa, sina mpango wa kuomba kazi, sitakuja kuandika barua yeyote ya kuomba kazi, hivyo sijaomba kugombea nafasi hiyo, ila kama kuna watakaoona ninafaa, sitawaangusha Waafrika,”alisema.
Alisema kutajwa kwa jina lake katika nafasi hiyo ni vizuri na iwapo atapendekezwa, hawezi kukimbia dhamana hiyo na atahakikisha anawakilisha vizuri katika kutetea maslahi ya nchi zinazounda umoja huo.
Dk. Kikwete pia alisisitiza haja ya Tanzania kuelekea katika nchi ya viwanda na kutokurudia makosa ya mataifa mengine katika tahadhari ya tabia nchi.
Akifungua mkutano huo, Dk. Kikwete aliwataka viongozi wa serikali, wafanyabiashara, taasisi zisizo za serikali na wadau wa mazingira, kuwekeza katika utafiti kwa ajili ya kutatua changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi.
Pia, alitoa wito kwa watafiti kuhakikisha wanatoa mchango mkubwa katika kuihadhari nchi na kushiriki kikamilifu katika mkakati wa kupambana na hali hiyo, kwa kuangalia zaidi tunu za mazingira ya Afrika na dunia.
“Nimetoa mawazo yangu juu ya hali mbaya iliyoko katika mabadiliko ya tabia nchi. Ilikuwa ni kilio changu cha muda mrefu kuona mkataba wa mapambano ya hali hii unafikiwa na hatimaye umesainiwa katika mji wa Paris. Ni vyema tuhakikishie tunatumia nafasi hii kuihadhari nchi kuelekea uchumi wa viwanda,”alisema.
Alisema matatizo ya tabia nchi ni ya kweli na Tanzania ni mfano wa nchi inayokumbwa na tatizo hilo na kwa sasa joto limeongezeka na kuathiri mifumo ya hali ya hewa, huku mvua za msimu zikiwa hazitabiriki, vimbunga na ukamwe vikiongezeka, hivyo ipo haja ya kuchukua hatua za haraka.
Alisema tatizo la mabadiliko ya tabia nchi ndilo linaloathiri zaidi sekta ya kilimo na hakuna njia ya kukabiliana na hali hiyo zaidi ya binadamu kuamua kuchukua hatua.
“Hali ni mbaya, theluji katika Mlima Kilimanjaro inaanza kupungua,kina cha bahari kinapanda, kwa watu wanaotumia visima kama mimi sasa hivi maji halisi yamepotea na kuwa maji ya chumvi, mji wa Pangani baada ya miaka 20, utapotea kabisa, lazima dunia kuchukua hatua,”alisema.
Alisema katika kipindi cha uongozi wake, amefanya kazi kubwa kuona mkataba huo wa mapambano ya mabadiliko ya tabia nchi unafikiwa, hivyo Watanzania waitumie fursa hiyo katika kuleta tija nchini.
No comments:
Post a Comment