RAIS Dk. John Magufuli amepongeza hatua ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kukubali sh. bilioni sita walizomkabidhi Aprili 11, mwaka huu, kutokana na mpango wa kubana matumizi, kuzielekeza kwenye oparesheni ya madawati bila kujali itikadi za vyama vyao.
Aidha, amesema mpango wa uchangiaji madawati umefanikiwa kwa zaidi ya asilimia 90, hivyo wadau mbalimbali waungane na serikali katika kuboresha miundombinu ya shule, hususani ujenzi wa madarasa.
Hata hivyo, Rais magufuli ameeleza kutoridhishwa na kasi ya utengenezaji madawati hayo, kazi inayofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Magereza nchini.
“Nawapongeza kwani watoto wanaokwenda kukalia madawati haya ni wanafunzi wa Tanzania, hawaonyeshi itikadi ya chama wala kabila,” alisema Rais Magufuli.
Alisema hatua hiyo inaunga mkono ahadi yake aliyotoa tangu wakati wa kampeni kuwa, iwapo atashinda uchaguzi, atawatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi za vyama vyao.
Alisisitiza kuwa ni vema kila mmoja akajikita katika utatuzi wa matatizo ya wananchi, badala ya kujali itikadi za chama chake na kulipongeza bunge kwa kuwa mfano mzuri.
“Tumetatua kwa kiasi kikubwa changamoto ya upungufu wa madawati, ambapo kwa shule za msingi, tumepata madawati milioni moja, sawa na asilimia 88.8 na kwa shule za sekondari, asilimia 95.8,” alisema.
Alifafanua kuwa upungufu kwa shule za msingi ulikuwa madawati milioni 1.4 na kwa shule za sekondari, ulikuwa madawati 188,850.
“Nimeridhishwa na mwitikio wa wadau mbalimbali katika uchangiaji madawati. Machi 15, mwaka huu, nilipowaapisha wakuu wa mikoa, niliwaagiza kwenda kushirikiana na taasisi mbalimbali, mashirika ya umma na watu binafsi kutatua changamoto hii,” alisema.
Alisema baadhi ya taasisi, ikiwemo Benki ya Tanzania (BOT) na mifuko ya hifadhi za jamii ya PPF na NSSF, bado haijawasilisha michango iliyoahidi.
“BOT iliahidi shilingi bilioni nne na kutangaza kabisa hadharani, lakini bado hawajaleta. Naamini watawasilisha na fedha zote nitazielekeza kwenye ukamilishaji wa mpango huu kama nilivyoahidi,” alisema.
Rais Magufuli alieleza kusikitishwa kwake na kasi aliyoiita ndogo ya utengenezaji wa madawati, ambapo alitoa sh. bilioni 50, kwa ajili ya madawati 120,000, lakini hadi sasa ni takribani madawati 60,000 tu yaliyokamilika.
“Simung’unyi maneno, nasema wazi kuwa sijaridhishwa na kasi yenu.
Nguvu kazi mnayo ya kutosha, fedha ipo, hamjihusishi na rushwa na ni taasisi za serikali, ninyi ndio mnafaa zaidi, lakini mnaniangusha, au mnataka niwape wengine kazi hii? Sitawapa bali muongeze kasi,” alisema Magufuli.
Alimwagiza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk. Hussein Mwinyi, Mkuu wa Majeshi, Meja Jenerali Davis Mwamunyange, na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, waliokuwepo kwenye hafla hiyo, kuhakikisha wanasimamia shughuli hiyo ili kuendana na kasi ya serikali.
“Makuruta ni wengi jeshini, mnayo nguvukazi ya kutosha. Kasi ya madawati 30, kwa kambi kwa siku moja haitoshi. Pia, magereza wapo wafungwa wengi na wengine watafungwa leo, hivyo nataka kasi ya utengenezaji wa madawati 60,000, yaliyosalia iongezeke,” aliagiza.
Hata hivyo, alisifu madawati yaliyotengenezwa na taasisi hizo mbili kuwa ni ya kiwango cha juu na ubora, ambapo aliahidi kuendelea kuvitumia vyombo vya ulinzi na usalama kwa shughuli mbalimbali.
Aidha, Rais Magufuli amewaomba Watanzania kuonyesha moyo katika kuunga mkono jitihada za utoaji elimu bure kama walivyofanya kwenye madawati, wafanye pia katika ujenzi wa madarasa.
“Kufuatia mpango wa elimu bure, udahili wa wanafunzi, hususani kwa shule za msingi, umeongezeka mara dufu ya awali, hivyo kuibua tatizo la uhaba wa madarasa, vyoo na nyumba za walimu, tuweke itikadi zetu pembeni na tushirikiane katika hili pia na nchi yetu itakuwa mfano wa maendeleo kwa nchi nyingine,” alisema.
Alisisitiza kuwa ataendelea kushirikiana na watu wa itikadi zote katika kuhakikisha taifa linakuwa na maendeleo kwa wote na kuinua maisha ya wanyonge.
Katika hafla hiyo, Rais Magufuli, aligawa madawati kwa baadhi ya majimbo nchini, ambapo alimkabidhi mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu, madawati 537 kwa niaba ya majimbo mengine.
Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson aliitaja mikoa itakayopatiwa madawati kwa awamu hii ya kwanza kuwa ni Pwani, Morogoro, Mtwara, Lindi, Ruvuma, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe, Rukwa, Katavi, visiwa vya Unguja na Pemba, Tanga na Dar es Salaam.
Alisema ugawaji wa madawati katika mikoa mingine utazingatia ukaribu wa maeneo yanapotengenezwa ili kupunguza gharama ya usafirishaji na kuepuka uharibifu.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akizungumza katika hafla hiyo, alimtaka rais kutokata tamaa katika kuwapigania Watanzania wanyonge.
Akipokea madawati hayo, Zungu alisema baada ya kupokea idadi hiyo, tatizo la madawati jimboni kwake limekwisha na leo anatarajia kukabidhi sh. milioni 27, kutoka mfuko wa maendeleo wa jimbo hilo kwa Makonda, kwa ajili ya kuchangia madawati katika shule za sekondari.
No comments:
Post a Comment