Wednesday, 13 July 2016

WANAFUNZI 2,379 WALIOOMBA MIKOPO KUHAKIKIWA UPYA

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imetoa siku saba kwa wanafunzi 2,379, wa vyuo vikuu nchini kujitokeza kuhakikiwa upya ili kutambulika kama wanazo sifa zinazostahili kupata mikopo.

Mbali na hilo, HESLB imesitisha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi hao kutokana na kutojitokeza kufanyiwa uhakiki na kwamba, watakaobainika hawastahili, watafutiwa mikopo yao na kurejesha kiasi cha fedha walichokwishakopeshwa.

Akizungumza jana, Dar es Saalam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Jerry Sabi alisema mchakato huo wa uhakiki ulifanywa na jopo maalum, lililoundwa na HESLB, kuanzia Mei 30, mwaka huu na kwamba bado inaendelea kuwahikiki.

Sabi alisema matokeo ya awali ya mchakato huo yalifanywa katika taasisi 26 na tayari zimehakikiwa, ambapo uchambuzi wa taasisi 18, umekamilika. Katika taasisi hizo 18, wanafunzi 2,739 hawakujitokeza kuhakikiwa.

"Katika wanafunzi hao, 763 wametoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), 126 kutoka Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino 232, Chuo Kikuu cha Mzumbe 66, Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji-Mbeya 130 na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino-Mbeya 21, " alisema.

Alivitaja vyuo vingine kuwa ni Chuo Kikuu cha Mkwawa 103, Chuo Kikuu cha Iringa 100, Chuo Kikuu cha Tiba-Bugando 43, Chuo Kikuu cha Arusha 55, Chuo Kikuu cha Jordan 128 na Chuo Kikuu cha Makumira-Arusha.

Wanafunzi wengine wametoka katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine 385, Chuo Kikuu cha Ufundi Arusha 22, Chuo Kikuu cha Kiislamu-Morogoro 130, Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha 57 na Chuo Kikuu cha Mount Meru 17.

Alisema uchambuzi wa awali wa vyuo vingine vinane unaendelea, ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es saalam (UDSM), Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yosefu, Chuo cha Biashara- Dar es Saalam, Chuo cha Bagamoyo, Chuo Kikuu cha Mwenge, Chuo cha Biashara- Dodoma na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi.

Sabi alisema endapo mchakato wa uhakiki utaonyesha kuwepo kwa dalili za wanafunzi hewa, italazimika kufanyika kwa uhakiki huo nchi nzima na kwamba mchakato huo ni wa awali.

"Orodha ya majina ya wanafunzi ambao hawakuhakikiwa wakati wa mchakato huu na wakati ukiendelea kwenye vyuo vingine, yapo kwenye tovuti ya bodi na yatatumwa vyuoni kwa ajili ya taratibu za uhakiki,"alisisitiza.

Alisema wanafunzi hao wanatakiwa kujitokeza katika muda wa siku hizo saba kuanzia Julai 13, mwaka huu. Aliongeza kuwa menejimenti za vyuo zinatakiwa kuratibu mchakato huo ili kukamilika ndani ya muda uliopangwa.

No comments:

Post a Comment