Wednesday, 13 July 2016
TETEMEKO LA ARDHI LATIKISA DODOMA
WAKAZI wa Mji wa Dodoma, jana, alfajili waliingiwa na taharuki baada ya mji huo kukumbwa na tetemeko la ardhi.
Tetemeko hilo lilitokea saa 12.03 asubuhi, wakati watu wengi wakiwa bado wamelalala.
Akizungumza na waandishi wa habari, ofisini kwake jana, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania, Profesa Abdulkarim Mruma, alisema tetemeko hilo lina ukubwa wa Rector 5.1.
Alisema tetemeko hilo ni kubwa, ikilinganishwa na matetemeko, ambayo yamezoeleka kutokea, ambayo yana ukubwa wa Rector 3.
“Hili ni tetemeko kubwa kwa hapa kwetu na hivyo ni lazima kuchukua tahadhari zaidi," alisema.
Aliongeza kuwa tetemeko hilo lilianzia katika bonde la Haneti - Itiso, wilayani Kondoa, kutokana na kupasuka kwa matabaka ya ardhi.
Kwa mujibu wa Profesa Mruma, kutokana na ukubwa wa tetemeko hilo, mikoa mingine, ambayo ipo karibu na eneo la chanzo cha tetemeko nayo itaathirika.
Alisema mikoa ambayo inaweza kuathirika ni pamoja na Tanga, Dodoma, Singida na Manyara.
Profesa Mruma alisema tetemeko hilo ni endelevu kwani bonde hilo la Itiso linazidi kusogea.
Aliwashauri watu wanaojenga maghorofa katika mkoa wa Dodoma, kuzingatia ushauri wa Wakala wa Jiolojia kwani athari za kujenga majengo marefu kwa mkoa huo bado zipo pale pale.
“Hivi sasa tunaona watu wanajenga maghorofa marefu hapa Dodoma, baadhi yao wanakuja kuomba ushauri, lakini wengine hawaji. Ukweli ni kuwa ukitaka kujenga ghrofa zaidi ya mbili ni lazima jengo liwe pana,"alisema.
Alisema ndiyo sababu katika Chuo Kikuu Cha Dodoma, hakuna jengo ambalo ni refu zaidi ya ghoarofa mbili, kutokana na kuomba ushauri kutoka kwa wakala huo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment