Thursday, 14 July 2016

MAJALIWA: TUTAJENGA VIWANDA VINGI



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akiwapungia wananchi wakati  akikagua ujenzi wa kiwanda cha vigae cha Goodwill Ceramic  kwenye kijiji cha Mkiu wilayani Mkuranga Julai 13, 2016,Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo  na kulia ni Balozi wa China nchini,  Dkt Lu Youqing. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya shilingi milioni 20 kutoka kwa Balozi wa China nchini, Dkt. Lu  Youqing   (wapili kulia) kwa ajili ya madawati wakati alipokagua ujenzi wa kiwanda cha vigage cha Goodwill Ceramic kinachojengwa katika kijiji cha Mkiu wilayani Mkuranga Julai 13, 2016.  Kushoto ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage,  Kushoto kwa Waziri Mkuu ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandishi Evarest Ndikilo na  kulia ni Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega. (Picha na Ofisi ya Wzri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa akipongezana na Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega baada ya kupokea hundi ya shilingi milioni 20  kutoka kwa Balozi wa China Nchini, Dkt. Lu Younqing kwa ajili ya madawati baada ya kukagua ujenzi wa kiwanda cha vigae cha Goodwill Ceramic kilichopo katika kijiji cha Mkiu wilayani Mkuranga Julai 13, 2016.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumzana Balozi wa China Nchini , Dkt. Lu Youqing (wapili kulia) , Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage (kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo (kushoto) baada kukagua ujenzi wa kiwanda cha vigae cha Goodwill na kuzungumza na wananchi kwenye kijiji cha Mkiu wilayani Mkuranga Julai 13, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha viwanda vinajengwa kwa wingi nchini kwani ndiyo msingi imara wa ukuaji wa uchumi na muarobaini wa tatizo la ajira hususan kwa vijana.

“Mbali na kukuza uchumi na kuongeza fursa za ajira nchini, viwanda hivi ndivyo vitakavyotufanya tununue bidhaa kwa bei nafuu tofauti na ilivyo sasa kwa kuwa vitu vingi vinaagizwa kutoka nje ya nchi,” alisema.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumatano Julai 13, 2016) wakati akikagua ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Goodwill Tanzania Ceramic katika kijiji cha Mkiu wilayani Mkuranga, Pwani.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Bw. Frank Yang alisema jumla ya ajira 4,500 zinatarajiwa kutolewa kiwandani hapo mara ujenzi utakapokamilika.

Akifafanua kuhusu ajira hizo Bw. Yang alisema ajira 1,500 zitakuwa rasmi na zisizo rasmi zitakuwa 3,000 huku wakazi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka kiwanda hicho wanatarajiwa kupewa kipaumbele.

Mkurugenzi huyo alisema ujenzi wa kiwanda hicho utagharimu dola milioni 100 na utafanyika kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza inatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.

“Ujenzi wa kiwanda hiki utainua ukuaji wa uchumi nchini  Tanzania kwani utakapokamilika Serikali itakusanya sh. bilioni 30 kwa mwaka ikiwa ni mapato ya kodi,” alisema.

Naye Balozi wa China nchini Tanzania Dk.Lu Youqing aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuchagua sekta ya viwanda kuwa ndiyo kipaumbele chake katika kukuza uchumi.

Alisema mbali ya ujenzi wa kiwanda cha vigae katika eneo hilo pia wawekezaji hao kutoka nchini China wanatarajia kujenga viwanda vya mbolea, karatasi na glasi (bilauli).

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alipokea msaada wa madawati 500 yenye thamani ya sh milioni 40 ambayo yalitolewa na Balozi wa China nchini Dk. Lu kwa kushirikiano na Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Goodwill Tanzania Ceramic Bw. Yang.

No comments:

Post a Comment