Tuesday, 12 July 2016

ANAYETUHUMIWA KUIBA MIL. 7 KILA DAKIKA KORTINI, ASOMEWA MASHITAKA 199


MFANYABIASHARA Mohamed Yusufali aliyetajwa na Rais Dk. John Magufuli kwa tuhuma za kuibia serikali sh. milioni saba kwa kila dakika moja, amepandishwa kizimbani na wenzake wakikabiliwa na mashitaka 199 yakiwemo ya kukwepa kodi na kuisababishia serikali hasara ya sh.bilioni 15.6.
Yusufali ambaye anajulikana kama Mohamedali au Choma au Jamalii peke yake alisomewa mashitaka 197 jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku wafanyabiashara wenzake wakisomewa mashitaka matatu.
Mfanyabiashara huyo na wenzake Alloyscious Mandago, Taherali Sujjauddin na Mohamed Kabula, walifikishwa saa 6.10 mchana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kupandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.
Yusufali na wenzake walifikishwa mahakamani hapo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 28 ya mwaka huu.
Mawakili wa Serikali Waandamizi, Shadrack Kimaro, Pius Hilla na Wakili wa TAKUKURU, Leonard Swai, walitumia takriban saa tatu kuwasomea washitakiwa hao mashitaka hayo huku wakipokezana.
Mfanyabiashara Yusufali alisomewa mashitaka 197 peke yake ya kughushi nyaraka kuonesha kampuni mbalimbali zilisajiliwa kihalali nchini na kuwasilisha nyaraka hizo za uongo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mkoa wa Kikodi wa Kinondoni, Dar es Salaam, kuonyesha zilisajiliwa kihalali na zinastahili kulipa kodi.
 Mashitaka mengine aliyosomewa mfanyabiashara huyo ni ya kughushi stakabadhi za malipo mbalimbali zenye thamani tofauti, kughushi marejesho ya kodi za ongezeko la thamani kwa miezi tofauti tofauti, kukwepa kodi ya sh. 15,645,944,361 kwa kuwasilisha marejesho hayo ya uongo, kutakatisha fedha na kuisababishia serikali hasara.
Akisoma mashitaka hayo, Wakili Kimaro alidai katika shitaka la kwanza hadi 30 yanayomkabili mshitakiwa huyo ni ya kughushi nyaraka za kuonesha kampuni mbalimbali zikiwemo za Festive General Business Limited,  Cebers General Co. Limited, Emi General Properties Limited, Fast Future General Trading Limited, Lotega General Co. Limited kuonyesha zimesajiliwa kihalali nchini.
Kampuni nyingine mshitakiwa huyo anazodaiwa kughushi nyaraka ni Great Lake Supplies Limited,  Lective General Co. Limited, Barents General Supply Limited, Dice Hardware & Building Material Limited, Raneys General Enterprises Limited, Akberali General Supply Limited, Adam General Trading Limited, Coat Blue General Co. Ltd, Real Way Logistice Co. Limited na Display Logistics Limited.
Pia mshitakiwa huyo anadaiwa kuwasilisha nyaraka hizo za kughushi katika ofisi za TRA, mkoa wa Kikodi Kinondoni, kuonyesha zimesajiliwa kihalali na zinastahili kulipa kodi.
Shitaka la 31 linawakabili Mandago na Kasanga ambao Oktoba 30, 1995, mkoani Dar es Salaam, kwa nia ya udanganyifu walighushi nyaraka za uongo kuonyesha kwamba kampuni ya Rafiki Commodities (T) limited imesajiliwa kihalali nchini.
Pia washitakiwa Sujjauddin na Kabula wanadaiwa Mei 16, mwaka 2011, mkoani Dar es Salaam, kwa nia ya udanganyifu walighushi nyaraka ya uongo kuonyesha kampuni ya Jambo Products (T) Ltd, imesajiliwa kihalali nchini huku wakijua si kweli.
Mfanyabiashara Yusufali alisomewa mashitaka mengine 73 ya kughushi stakabadhi za malipo kuonyesha kampuni ya Farm Plant Ltd imenunua bidhaa mbalimbali zenye thamani tofauti kutoka katika kampuni nyingine.
Timu hiyo ya mawakili wa serikali, ilimsomea mfanyabiashara huyo Yusufali mashitaka mengine ya kughushi marejesho ya ongezeko ya kodi ya thamani kwa miaka tofauti kuonesha kampuni hiyo Farm imenunua bidhaa zenye thamani tofauti.
Mfanyabiashara Yusufali anadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari 2008 na Januari mwaka huu, Dar es Salaam, akiwa mkurugenzi anayehusika na uongozi katika kampuni ya Farm Plant Limited ambayo imesajiliwa kama inalipa kodi, akiwa na nia ovu ya kukwepa kodi aliwasilisha marejesho ya uongo ya ongezeko la kodi ya thamani kwa Kamishna Mkuu wa TRA, hivyo kusababisha kukwepa kodi ya sh. 15,645,944,361.
Yusufali, Mandago, Kasanga, Sujjauddin na Kabula wanadaiwa tarehe tofauti kati ya Machi 2011 na Januari, mwaka huu, Dar es Salaam, wakiwa wahusika wa kuendesha kampuni ya Superior Financing Solution Limited, walificha uhalisia, chanzo na hata uhamishaji wa sh. 1,895,885,000 kwa kuzikopesha kwa watu mbalimbali na kisha kuzipokea, huku wakifahamu zilikuwa ni zao la makosa makubwa ya wizi ya kughushi na kukwepa kodi.

Shitaka la 199 linamkabili mfanyabiashara Yusufali ambaye anadaiwa tarehe tofauti kati ya Januari, 2008 na Januari, mwaka huu, kwa vitendo vyake viovu kwa kughushi na kuwasilisha marejesho ya uongo ya ongezeko la kodi ya thamani aliisababishia serikali hasara ya sh. 15,645,944,361 ambayo ilitakiwa kulipwa kama kodi ya ongezeko la thamani.
 Wafanyabiashara hao ambao walikuwa wanatetewa na mawakili takriban watano wakiwemo Hudson Ndusyepo,  Richard Rweyongeza, Michael Ngalo, hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi.
Wakili wa Serikali Hilla alidai upelelezi haujakamilika na kuomba shauri hilo kuahirishwa hadi tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 25, mwaka huu na kusema washitakiwa watarudi rumande.

No comments:

Post a Comment