Tuesday, 12 July 2016

MAGUFULI AWATWISHA MZIGO MZITO MA-DED




RAIS Dk. John Magufuli ametoa maagizo mazito kwa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri (DEDs), ikiwemo kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mashine za kielekroniki EFD ili kuziba mianya ya upotevu wa fedha za umma.
  
Mbali na hilo amewataka kutokubali kuburuzwa na madiwani katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuwa wapo wanaotumia nafasi hizo kutaka kunufaika na miradi mbalimbali.

Aidha, ameonya matumizi nje ya malengo kwa fedha za elimu zinazotolewa na serikali yake na kwamba, yeyote atakayebainika kuhusika rungu litamwangukia.

Amesema ametumia miezi mitatu kupitia jina na sifa ya kila mkurugenzi, hivyo wote aliowachagua wamekidhi vigezo na kwamba hana mashaka nao.

“Mhakikishe mnakusanya mapato ya fedha mbalimbali za miradi kwa uadilifu. Serikali imekuwa ikishinikiza matumizi ya EFD kwa wafanyabiashara peke yake, wakati fedha nyingi za umma zikipotea kutokana na serikali yenyewe kutotumia mashine hizo,”alisema.

Rais Magufuli aliwataka makatibu wakuu wa wizara zote, kuanzia sasa kuhakikisha wanasimamia matumizi ya EFD katika makusanyo ya fedha za umma.

Pia, amewataka wakurugenzi hao kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo na kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), badala ya kuburuzwa na madiwani, hususani katika ujenzi wa miundombinu.

“Serikali itatoa fedha nyingi katika mfuko wa barabara kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu katika halmashauri zenu, mtashangaa kuona madiwani wote ni wahandisi, msirubunike, fanyeni kazi kwa uadilifu na uwazi kwa kutangaza zabuni kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Aidha, aliwaagiza kusimamia na kuhakikisha ushuru wa mazao, hususani kwa wakulima wadogo unafutwa.

“Serikali hii ipo kutatua kero mbalimbali za wananchi na si kuwatelekeza, mpaka sasa bado kuna wakulima wadogo wanaonewa, wakilima mazao kidogo, wanatakiwa kulipa ushuru kana kwamba walisaidiwa kununua mbolea na maji ya kumwagilia, huo ni uonevu,” alisema.

Alisema miongoni mwa mafanikio, ambayo serikali ya awamu ya tano imefanikiwa ni mpango wa utoaji elimu bure, ikiwemo kutatua tatizo la madawati kwa asilimia 80.

“Serikali inapeleka jumla ya shilingi bilioni 18.77 kwa ajili ya maendeleo ya elimu, hivyo hakikisheni mnaboresha miundombinu, hususani ujenzi na ukarabati wa majengo,” alisema.

“Tayari zipo tetesi za ubadhirifu kwa baadhi ya wakuu wa shule, hivyo hakikisheni mnawabaini na hatua za haraka zichukuliwe kwa watakaobainika,” alisema.

Alisema ameteua kwa umakini mkubwa wakurugenzi hao na kwamba maneno ya upinzani yanayotolewa, yanaashiria kazi nzuri aliyoifanya ya uteuzi huo, usio na upendeleo wowote.

Aliwataka kutomwangusha, badala yake wakatende haki, wasimwonee wala kumpendelea mtendaji yeyote katika halmashauri zao.

“Mshirikiane vema na viongozi wa juu na chini yenu katika kutatua changamoto mbalimbali, hususani wakuu wa wilaya, ambao ndio wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama za wilaya husika,” alisema Rais Magufuli.

SAMIA ATOA NASAHA

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliwataka wakurugenzi hao kutambua kuwa wao ni watumishi wa umma na sio watawala, hivyo aliwataka kwenda kufanya kazi badala ya kuwa ‘miungu watu’.

“Mkifika maeneo yenu ya kazi, hakikisheni mnajifunza na kupitia wajibu wenu kisheria, huku mkifanya kazi kwa kasi kwa kuwa serikali hii inakwenda kwa kasi,” alisema Samia.

Aliwataka kuhakikisha fedha wanazokusanya zinatumika kwa manufaa ya Watanzania na si kujinufaisha wao.

MAJALIWA AWATAKA WACHAPE KAZI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliwaasa kuwa sifa ya DED ni uchapakazi, uadilifu na uaminifu, ambapo wao ndio kiini cha maendeleo ya nchi kupitia halmashauri zao.

Aliwataka wakurugenzi watendaji hao wa halmashauri, kuhakikisha wanatoa taarifa juu ya mapato na matumizi ya fedha za maendeleo zinatoka serikalini, ikiwemo kusimamia kikamilifu miradi iliyopo katika halmashaiuri zao.

“Lipo tatizo juu ya thamani ya fedha kutoendana na manunuzi husika, nawaagiza mhakikishe matumizi yanaendana na thamani ya fedha zilizoainishwa na sio vinginevyo,” alisema Majaliwa.

Aliwataka kuhakikisha wanafunzi wote, ikiwemo wa shule za msingi na sekondari, wanakaa kwenye madawati badala ya kukaa chini.

Waziri Mkuu aliahidi kuwatembelea kila mara, ikiwa ni moja ya jukumu lake la kusimamia utendaji na utekelezaji wa majukumu yao.

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia, akizungumza katika hafla hiyo, aliahidi kusimamia  miradi mbalimbali iliyopo katika jiji hilo kwa kiwango kizuri kwa kushirikiana na wadau wote.

Kihamia alisema atahakikisha suala la watumishi hewa linabaki historia katika jiji hilo, ikiwemo kusimamia vema fedha za elimu, ambazo zinatolewa na serikali.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Simanjiro, Ayub Nyenzi, ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki Ardhi, alisema atahakikisha kuwa migogoro ya ardhi inatatuliwa katika halmashauri yake.

"Nimeitumikia sekta ya ardhi kwa miaka 15, hivyo huu ni wakati muafaka kutatua changamoto zilizopo wilayani kwangu kwa ushirikiano na wenzangu," alisema.

Aidha, alisema atatumia taaluma yake ya utawala ili kuhakikisha anarejesha misingi ya utawala bora kwa watumishi katika wilaya hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Muheza, Luiza Mlelwa, alisema atahakikisha anasimamia mapato ya wilaya yake ili kutatua changamoto kwa wakati.

No comments:

Post a Comment