MWENYEKITI wa Jumuia ya Wazazi Taifa (CCM), Abdallah Bulembo amekanusha vikali kuhusika na tuhuma za ‘kufungwa mdomo’ kwa fedha ili asifuatilie mgogoro wa eneo la uwanja wa Sanaa, ulioko Shekilango, Ubungo, Dar es Salaam.
Katika tuhuma hizo zilizochapishwa juzi na gazeti moja la kila siku (sio Uhuru), ilidaiwa kuwa Bulembo alipokea sh. milioni 100, kutoka kwa mfanyabiashara mmoja hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari, mjini Dar es Salaam, jana, Bulembo alisema kamwe hahusiki na tuhuma hizo na kama kuna mtu yeyote mwenye ushahidi na jambo hilo, achukue hatua za kisheria dhidi yake badala ya kutapatapa kupitia kwenye vyombo vya habari.
“Wewe unauliza suala la Shekilango, mimi sitaki kuzungumzia hilo kwa sababu halina tija kwangu, lakini kwa kuwa umeuliza basi nitakujibu kidogo.
“Binafsi sihusiki na tuhuma hizo, ni vizuri tukaviachia vyombo husika kama vile TAKUKURU vifanye kazi yake na ikithibika nitawajibika,” alisema Bulembo.
Alisema anashangaa kutupiwa tuhuma za ‘kupikwa’ badala ya kumpongeza kwa jitihada alizozifanya za kupigania haki katika eneo hilo.
“Kwa kiongozi wa juu kama mimi kupigwa ‘madongo’ ni jambo la kawaida sana, wala sishangai. Kesi ya Shekilango ina miaka 18 sasa. Mimi niliikuta kutoka kwa watangulizi wangu.
“Eneo lile naliheshimu sana maana tulipewa na muasisi wetu mama Maria Nyerere, kuonyesha upendo wake kwa jumuia yetu, iweje leo niingie mtegoni kwa kitu chenye historia ya wazi katika nchi hii?”Alihoji Bulembo.
Alisema mgogoro wa eneo la Shekilango unashughulikiwa na vyombo halali vya kisheria na kwamba, hawezi kuingilia uhuru wa vyombo hivyo.
Alifafanua kuwa uongozi wake wakati ukiingia madarakani, ulikuta kesi zaidi ya 60 na ilipambanazo nazo na kubakisha takriban nusu yake na kupata mafanikio makubwa, lakini wabaya wake hawatambui jitihada hizo, badala yake wamekuwa wakitumia nguvu nyingi kumchafua.
No comments:
Post a Comment