Tuesday, 12 July 2016
TISA MBARONI KWA KUKUTWA NA MENO 666 YA TEMBO
JESHI la Polisi nchini limewakamata watu tisa, wakiwemo raia wawili wa Uganda na Guinea, wakiwa na vipande 666, vya meno ya tembo, vyenye uzito wa kilo 1,279.19, vyenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni 4.6.
Pia, limekamata madini aina ya Acquamiline Smoky, yenye uzito wa kilo 20 na kubaini uwepo wa kampuni tatu zinazojishughulisha na biashara ya madini huku zikikosa uhalali wa kumiliki leseni ya biashara hiyo.
Aidha, watuhumiwa 265, wamekamatwa kwa tuhuma mbalimbali, kufuatia msako uliofanywa na jeshi hilo kwa ushirikiano na Polisi wa Kimataifa (INTERPOL) Kanda ya Kusini mwa Afrika (SARPCCO).
Akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, jana, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa jeshi hilo, Kamishna, Diwani Athumani, alisema msako huo ulifanyika nchi nzima kwa kuzihusisha pia idara na taasisi mbalimbali za serikali.
Alisema vipande hivyo vya meno ya tembo vilikamatwa kufuatia taarifa za kiintelejensia, wakati wa matayarisho ya operesheni hiyo.
Aliongeza kuwa kulingana na hali halisi ya taarifa hizo, iliwalazimu maofisa wa kikosi maalumu kuyakamata meno hayo siku nne kabla ya kuanza kwa operesheni.
“Maofisa wa Task Force (Kikosi kazi maalum), ilibidi wayakamate siku nne kabla ya tarehe ya operesheni ili kuepuka watuhumiwa kutoroka au kuyatorosha meno hayo,” alisema Kamishna Athumani.
Alibainisha kuwa katika msako huo, pia walifanikiwa kubaini kampuni tatu za madini, ambazo ni Delicore Metal, Madandwa Gold Mining Export Import na Adex Mining, ambazo hazina sifa ya kuwa na leseni ya kufanya biashara hiyo.
Alisema suala hilo tayari limeshakabidhiwa katika Wizara ya Nishati na Madini ili lifanyiwe kazi zaidi.
Aidha, katika msako huo, wahamiaji haramu 43, walikamatwa, kati yao
18, ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), 22 kutoka Burundi, wawili kutoka Uganda na mmoja raia wa Kenya.
Kamishna Athumani alisema pia kuwa risasi 104, bunduki moja aina ya Shortgun, magobore 11, milipuko 15 pamoja na mkuki ilikamatwa kwenye msako huo.
Pia, alisema walifanikiwa kukamata magari 10, yaliyoibwa katika
nchi mbalimbali, ambapo matatu yaliibwa Afrika Kusini, matano yaliibwa Uingereza, Malaysia yaliibwa magari mawili huku mengine matano yakiendelea kufanyiwa uchunguzi.
Aliongeza kuwa pikipiki 12, zilibainika kuibwa huku 18, zikiwa bado zinafanyiwa uchunguzi ili kubaini uhalali wa umiliki wake.
Aliwaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za matukio mbalimbali ya kiharifu ili kuliwezesha jeshi hilo liweze kukabiliana na vitendo hivyo vinavyohatarisha usalama wa raia na mali zao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment