Tuesday 12 July 2016

POLISI WAMNASA ASKOFU GWAJIMA

JESHI la Polisi limemkamata na kumuhoji kwa saa kadhaa, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam, wakati akirejea nchini.

Askofu Gwajima alikamatwa jana, saa nne asubuhi, alipowasili uwanjani hapo akitokea nje ya nchi.

Akithibitisha kukamatwa kwake, Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Martin Otieno, alisema Askofu Gwajima alikamatwa muda huo na baadae kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati (Central), ambako alihojiwa.

"Taarifa za kukamatwa kwa Gwajima ni za kweli. Tulimkamata baada ya kutua na ndege ya Shirila la Ndege la Kenya (KQ)," alisema.

Kwa upande wake, Mchungaji Msaidizi wa kanisa hilo, Yekonia Bihagaza, alikiri kukamatwa na kushikiliwa kwa muda kwa Gwajima, ambaye alisema alikuwa akirejea nchini kutoka kwenye shughuli za kiutumishi za kuhubiri Injili katika nchi za Ulaya.

Alisema Askofu Gwajima hakuwepo nchini kwa muda mrefu kidogo na kwamba, safari yake ni ya kawaida katika shughuli za kuhubiri, ambazo humfanya asafiri kwenda nje mara kwa mara ili kutekeleza majukumu yake.

"Taarifa za kukamatwa kwa Askofu Gwajima nimezipata, lakini nilikuwa mbali kidogo, hivyo sikubahatika kwenda kituo kikuu cha polisi,
lakini alikuwepo mwanasheria wake, ndiye anafahamu kinachoendelea huko,"alisema.

Wakili wa Askofu Gwajima, Peter Kibatala, alithibitisha kukamatwa kwa Gwajima na kufikishwa kituo cha kati cha polisi, ambako alihojiwa kwa muda mfupi kisha kuachiwa huru.

"Ni kweli alihojiwa na baadae kuachiwa huru. Ninachokifahamu ni hicho na kwa leo naomba nifafanue hiki ninachosema, kama kutakuwa na kingine nitawajulisha,"alisema.

Alisema Askofu Gwajima amejidhamini mwenyewe na baada ya hapo aliachiwa huru kutokana na kufanikiwa kuwa na vigezo vya kupata dhamana.

Juni 18, mwaka huu, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Saalam, Simon Sirro aliwataka watu wenye taarifa juu ya mahali aliko Askofu Gwajima, awasaidie polisi kwa kuwa bado wanaendelea kumtafuta.

Askofu Gwajima alikuwa akitafutwa kwa siku 22, kipindi ambacho mkanda unaodhaniwa kuwauna sauti yake, umezagaa kwenye mitandao ya kijamii.

Sauti hiyo iliyo kwenye mkanda huo, inatamka Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, afikishwe mahakamani kwa yote yaliyofanyika wakati wa utawala wake.

No comments:

Post a Comment