Wednesday 3 August 2016

MREMA AMVAA LOWASSA

MWENYEKITI wa Bodi ya Parole, Augustine Mrema amemvaa Edward Lowassa,  huku akiwataka madereva wa bodaboda kutokubali kutumika kisiasa kwa sababu muda wake umepita.

Amesema madereva hao hawapaswi kufungamana na upande wowote kisiasa na kwamba, wakati huu wautumie kuboresha uchumi wao na familia zao.

Akizungumza na madereva hao jijini Dar es Salaam, jana, Mrema alisema tabia ya baadhi ya wanasiasa, hasa wa upinzani kuwatumia madereva hao kwa manufaa yao binafsi waikatae.

Alisema kipindi cha vuguvugu la kisiasa kutafuta dola kimepita, ambapo kutokana na shamrashamra, iliwabidi madereva hao kujumuika na upande fulani, hivyo wakati huu ni wa kuiunga mkono serikali iliyoko madarakani.

Mrema alisema amesukumwa kuzungumza na madereva wa bodaboda kutokana na umuhimu wao kwenye masuala ya usalama katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Alisema serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, inafanya kazi nzuri, ambapo aliwataka waendesha bodaboda wa wilaya ya Kinondoni waiunge mkono kwenye kuchapa kazi kwa maendeleo ya nchi.

Kundi hilo,  Mrema alisema kadri siku zinavyokwenda, linazidi kuongezeka, hivyo linapaswa kujitahidi kuepukana na kuchanganywa na wanasiasa, jambo ambalo litawachonganisha na serikali yao.

“Vijana nimekutana nanyi kwa lengo la kuwakumbusha kuwa ninyi ni sehemu muhimu kwa usalama wa nchi, mnaye rais mzuri, mkiwa waoga shauri yenu, toeni malalamiko yenu kwa ustaarabu atawasaidia,” alisema.

Mrema alitumia fursa hiyo kusema kuwa wanaodai yeye ni CCM B, wameishiwa na hoja kutokana na ukweli uliopo kuwa, ana miaka zaidi ya 30, tangu alipoondoka kwenye chama hicho huku wanaomuita wakiwa na miezi tu.

“Nimeondoka CCM mwaka 95, wewe umeondoka juzi baada ya kula, nani CCM B? Tuache unafiki, Rais Magufuli wakati anafanya kampeni, nilichambua nikaona yeye ndiye anafaa kwa taifa letu, kwanini nisimuunge mkono?” Alihoji.

Alisema Rais aliyeko madarakani ni Dk. John Magufuli na hakuna mwingine hadi atakapochaguliwa mwingine 2020, hivyo hakuna namna wala maana ya kupingana na uongozi uliochaguliwa na umma.

Alisema yeye anaipenda Tanzania, hivyo hayuko tayari kuwa mnafiki ili kupendwa na kundi fulani la watu, ambao hawana mapenzi mema na nchi yao.

“Nilivyoondoka CCM, nilimtaka Lowassa (Edward) anifuate akakataa, nikaongea na Sumaye na yeye akagoma wakabaki… nikatoka, nikawa na nguvu kuliko, lakini CCM haikung’oka. Wao ni nani, leo waing’oe? Kama ni CCM kutoka ilikuwa 1995 si leo,” alisema. 

Pamoja na hilo, Mrema alisema amejitolea kufanya kazi aliyopewa na Rais Dk. Magufuli kuwatumikia wananchi kuanzia ngazi ya chini na si kwenye magereza, mahabusu kama walivyodai baadhi ya mahasimu wake.

Kuhusu kufurika kwa magereza na mahabusu, Mrema alisema vijana na umma kwa ujumla wanatakiwa kuhakikisha wanatii sheria bila shuruti ili kuepuka kushikwa na vyombo vya dola.

“Tuheshimu sheria, tuzuie vitendo vinavyozalisha mahabusu na wafungwa… tunazuiaje? Nimeanza kuzungumza nanyi kabla hata ya kwenda kwenye hizo mahabusu na magereza, tunaweza,” alisema.

Awali, akisoma risala yao kwa kiongozi huyo, Katibu wa Madereva wa Bodaboda Wilaya ya Kinondoni, George Mbwale, alisema changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni baadhi ya wanasiasa kuwatumia kwenye shughuli zao ikiwemo maandamano.

Aidha, alisema changamoto nyingine wanayohitaji serikali iwatatulie ni uwepo wa askari wanaokwenda kinyume na utaratibu wa utumishi wao kwa kuendekeza rushwa kutoka kwa madereva hao.

Alisema changamoto hiyo ni kubwa, ambapo askari hao huwakamata hata eneo ambalo dereva hajavunja sheria.

Kutokana na hilo, Mrema aliwapa siku saba madereva hao kupeleka orodha ya majina ya askari, ambao wanachukua rushwa ili majina hayo ayapeleke kwa Rais Dk. Magufuli.

No comments:

Post a Comment