Wednesday 3 August 2016

WANASIASA WAIONYA CHADEMA

CHADEMA imeonywa kuacha kuleta vurugu kwa kulazimisha maandamano, badala yake  imetakiwa kupeleka hoja za malalamiko yao kwenye Baraza la Vyama vya Siasa, ambalo lipo kisheria.

Pia, chama hicho kimeelezwa kuwa, nchi haiwezi kuendeshwa kwa kutunishiana msuli, badala yake sheria lazima zifuatwe ili kuiepusha kuingia kwenye machafuko.

Hayo yalielezwa na Mjumbe wa Kamati ya Uongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa, Constantine Akitanda, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Baragumu, kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Chanel Ten, Dar es Salaam, jana.

Pamoja na kauli hiyo, tayari Rais Dk. John Magufuli ameonya kuwa hataki kujaribiwa na kwamba, hataki nchi iwe ya vurugu na watakaoleta vurugu atawashughulikia kikamilifu bila huruma na wasije wakamjaribu.

Akitanda alisema suluhu ya jambo lolote ni kufanya majadiliano ili kufikia mwafaka, hivyo kitendo cha CHADEMA kutaka kulazimisha maandamano, hakina nia njema katika mustakabali mwema wa nchi.

“ Baraza la Vyama vya Siasa linaundwa na wajumbe 44, kutoka vyama 22, vya siasa na lipo kwa mujibu wa sheria, hivyo hakuna shaka kwamba wajumbe hao watashindwa kujadiliana na kufikia mwafaka ulio bora,”alisema.

Alisema hata katika uchaguzi mkuu uliopita, baraza lilikaa na kujadiliana mambo mbalimbali na ndiyo chanzo cha uchaguzi huo kwenda salama bila vurugu.

Kwa mantiki hiyo, alishauri chama chochote chenye malalamiko, kupeleka hoja zao kwenye baraza ili ziweze kujadiliwa na wajumbe na kupata mwafaka na ambaye hataridhika, akate rufani kwa ngazi zingine zaidi.

Aidha, Mshauri wa Kamati ya Uongozi wa baraza hilo, Martin Mung’ong’o, alishauri serikali kuliwezesha baraza hilo ili liweze kukutana mara kwa mara kujadiliana mambo yanayojitokeza katika nyanja za kisiasa nchini.

“Kama kukiwa na utamaduni wa kupeleka hoja za malalamiko ya vyama vya siasa kwenye baraza, hata Maalim Seif Sharifu Hamad asingekimbilia kwenye mahakama ya kihalifu,The  Hague, badala yake angeleta malalamiko kwenye baraza na kujadiliana,”alifafanua.

Baraza la Vyama vya Siasa ni chombo kilichoanzishwa na Bunge kwa Sheria ya Vyama vya Siasa namba tano na marekebisho ya saba yalifanyika mwaka 2009.

Majukumu ya baraza mbali ya kumshauri msajili wa vyama vya siasa,  changamoto na matatizo yanayotokana baina ya vyama, lina wajibu wa kuishauri serikali kupitia msajili wa vyama kuhusu utekelezaji wa majukumu ya kisiasa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa.

Hivi karibuni, CHADEMA ilitangaza kuanzisha operesheni UKUTA, ambapo wamelenga kuzunguka nchi nzima kueleza wanachama na wafuasi wao kwamba serikali imekataza mikutano ya kisiasa.

Hata hivyo, Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka, ameshaeleza kuwa, operesheni inayotajwa kutaka kufanywa na CHADEMA, imefadhiliwa na wakwepa kodi na wahujumu uchumi waliobanwa  mianya yao.

“Wapinzani wanataka kutunga uongo ili waendelee kupata wafuasi huku wakijua kwamba, serikali haijazuia mikutano ya kisiasa, kwani wabunge wapo huru kufanya mikutano kwenye majimbo yao yote, lakini tunajua wanataka kuwatetea wahujumu uchumi na wakwepa kodi,”alisema Sendeka.

No comments:

Post a Comment