Wednesday 3 August 2016

JPM AMALIZA MGOGORO WA MAKAZI MAGOMENI KOTA



SERIKALI inatarajia kuanza ujenzi wa nyumba za kisasa 640, eneo la hekta 33, lililovunjwa nyumba la Magomeni Kota, Dar es Salaam, ambapo itatoa kipaumbele kupangisha ama kuuza kwa wakazi walioondolewa katika eneo hilo.

Aidha, Rais Dk. John Magufuli, ameamua kurudisha hodhi ya eneo hilo na maeneo kama hayo yaliyokuwa yanamilikiwa na halmashauri za wilaya kote nchini, kwa serikali kuu, kutokana na halmashauri hizo kushindwa kuyaendeleza makazi hayo.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi, akizungumza jana, jijini Dar es Salaam, alisema serikali imeingilia kati mgogoro huo kutokana na Halmashauri ya Kinondoni kushindwa kutimiza mkataba na wananchi hao.

“Nimeshaagiza timu ya watendaji wangu kwenda kukagua na kuandaa eneo hilo tayari kwa kuanza ujenzi, ambao tunatarajia utachukua muda wa mwaka mmoja kukamilika,” alisema.

Alisema Rais Magufuli amechukua hatua hiyo kwa kuzingatia kilio cha wanyonge, ambao walikata tamaa juu ya hatima yao. Awali, serikali kuu ndio ilimiliki makazi hayo takribani nyumba 5,560 nchini.

“Mwaka 1991, ilihamishia umiliki kwa halmashauri husika kote nchini ili ziyaboreshe, jambo ambalo zimeshindwa na badala yake kuwaondoa wakazi kiholela. Nimewaagiza wakuu wa mikoa  20, zilipo nyumba hizo kutathmini na kurudisha umiliki kwa serikali kuu,” alisema.

Aidha, Lukuvi alisema serikali imeamua kufuta mikataba yote, ambayo Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni iliingia katika ardhi ile na kusisitiza kwamba, kwa sasa iko wazi tayari kwa kuanza ujenzi huo.

Kuhusu suala la malipo kwa wakazi watakaokuwa tayari kununua nyumba eneo hilo, alisema serikali imekusudia kutoza gharama za nyumba tu, ambapo wananchi watapatiwa hati zitakazomaanisha umiliki ardhi pia.

“Tutakaa na kukokotoa gharama za uuzaji nyumba hizo, zitakazokuwa na vyumba vitatu kwa wakazi wa awali na tunakadiria itakuwa  kati ya sh. milioni 50 na 60,” alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Wakazi wa Magomeni Kota, George Abel, aliishukuru serikali, hususani Rais Dk.  Magufuli na wizara hiyo na kusema imewafanyia kitu kikubwa, ambacho hawatakisahau maishani.

Mwanasheria wa wakazi hao, Twaha Taslima, alimsifu Rais Dk. Magufuli na kusema hakika serikali ya awamu ya tano ni ya vitendo, hivyo anaamini sasa taifa litaendelea kwa kuwa vitendo ndivyo huleta maendeleo kote duniani.

No comments:

Post a Comment