Friday, 18 November 2016

DK. SHEIN AMEWAUMBUA WAPINZANI- WASOMI


WASOMI na wanasiasa wamesema hatua ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dk.Mohamed Ali Shein kutia saini muswada wa sheria ya uchimbaji mafuta na gesi asilia, imewaumbua wapinzani waliokuwa wanapotosha ukweli.

Wamesema kitendo hicho kimeonyesha uhalisia kuwa Zanzibar inajiendesha yenyewe na kwamba, uamuzi huo umewambua wapotoshaji hao.

Wakizungumza na gazeti hili jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa,Profesa Benson Bana, alisema Dk. Shein ameonyesha kuwa Zanzibar inajiendesha yenyewe.

Profesa Bana alisema muswada huo umekuja wakati muafaka katika kuhakikisha Serikali ya Zanzibar inajiendesha yenyewe na kwamba, kitendo cha kutia saini muswada huo mbele ya umma ni ukomavu.

Aliongeza kuwa, Dk.Shein amewaumbua wapotoshaji, ambao wamekuwa wakipotosha ukweli kuhusu rasilimali hizo za mafuta na gesi asilia kuwa Zanzibar haihusiki nazo.

“Ni hatua nzuri na kwamba, rasilimali hizo zitaleta manufaa kote kuanzia visiwani na bara, hivyo ni jambo jema,”alisema.

Naye Profesa Hosea Kuyumbo kutoka Idara ya Sayansi ya Chuo Kikuu cha Dar es Saalam (UDSM), alisema Dk. Shein ametekeleza makubaliano yaliokuwepo katika Muungano.

Alisema miaka zaidi ya minane iliyopita, kulikuwa na mambo ya utata kuhusu Muungano, ambapo mafuta na gesi asilia ilikuwa mojawapo na sasa Dk. Shein ametimiza ndoto hiyo.

Profesa Kuyombo alisema suala la mafuta na gesi asilia limefikiwa hatua nzuri, ambapo miaka ya nyuma, walitumwa watafiti kwenda kuangalia mipaka baina ya Zanzibar na Bara ili kujua mafuta na gesi viko wapi.

“Zamani tulikuwa hatujui mipaka ya Zanzibar, hivyo baada ya wataalamu kubaini zaidi ya kilomita 200, kwenye Bahari ya Hindi, ndipo imefikia hatua nzuri kama tunavyoiona leo kusainiwa kwa sheria hiyo,”alisema.

Profesa Kuyombo alisema kitendo hicho cha kusainiwa kwa sheria hiyo kitasaidia kusafirisha mafuta ghafi katika maeneo ya bara, hususan Tanga kwenye bomba la mafuta kutoka Uganda.

Alisema fursa ya kuwepo kwa sheria hiyo, itasaidia kukuza uchumi wa Zanzibar kwa kuuza mafuta hayo katika nchi za Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo(DRC) na Burundi.

Mhadhiri huyo alisema Zanzibar itakuwa na fursa ya kuchimba mafuta ghafi na kuuza nchi hizo, ambapo kwa sasa pipa moja la mafuta hayo ni Dola 30 hadi 28 za Marekani.

“Ni jambo la kumpongeza Dk.Shein, lakini kinachotakiwa ni kuwa makini kisoko kwa sababu nchi za karibu nazo zinachimba kama vile Uganda,”alisema.

Katika hatua nyingine, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umeipongeza hatua hiyo na kufurahishwa na msimamo imara wa Dk.Shein kwa kufanikiwa kuliondoa suala la mafuta na gesi katika orodha ya mambo ya Muungano.

Katibu wa Idara ya Hamasa, Sera, Utafiti na Mawasiliano, Mtemi Sylivester Yared, amesema kwa kusaini muswada huo, Dk. Shein hakuvunja wala kukiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Mtemi Yared amesema wananchi wanapaswa kuwapuuza wanasiasa uchwara, wanaopita na kueneza upotoshaji na uzushi mitaani .

Mtemi Yared alisema kilichofanywa na Serikali ya Mapinduzi ni kuzima na kuizika zama ya maneno mengi, iliyomtaka Rais Dk. Shein kutosaini sheria hiyo.

Kaimu katibu huyo alisema kimsingi sheria hiyo itafungua fursa na milango kwa kampuni mbalimbali duniani, kujitokeza na kuanza kazi ya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia visiwani Zanzibar bila kuwepo urasimu.

Alisema kwa muktadha huo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo ilitakiwa  kuanzisha sheria yake yenyewe, ambayo itasimamia shughuli kama hizo kwa Zanzibar.

“Tunajua wanaopinga maendeleo, maadui wa Mapinduzi na Muungano, wamezidiwa kete, hawataacha kulalama ili kutimiza ada ya uzandiki kwao," alisema.

TADEA YAUNGA MKONO SMZ

Wakati huo huo, Chama cha ADA Tadea, kimesifu uamuzi na ujasiri wa Dk. Shein, kutia saini sheria hiyo mpya ya utafutataji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.

Chama hicho kimesema hatua hiyo haijavunja wala kukiuka sheria na katiba, kwa sababu suala hilo tayari limeondolewa kwenye orodha ya mambo ya Muungano.

Kimeelezea matumaini yake kwa kitendo hicho na kuwataka Wazanzibari waendelee kutii sheria, kuenzi amani, umoja na utulivu na kwamba, hali ya umasikini na unyonge wa vipato itatoweka

Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa Tadea, Rashid Yussuf Mchenga, alisema kitendo hicho hakivunja Katiba ya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.

Alisema kwa muda mrefu chama upinzani cha Zanzibar (CUF) na viongozi wake, wamekuwa wakipiga mayowe ya kutaka suala la mafuta na gesi asilia liondolewe kwenye  orodha ya mambo ya Muungano, jambo ambalo sasa Dk. Shein amelikamilisha.

"Bunge la Muungano limeridhia kuondolewa suala la mafuta na gesi katika orodha ya mambo ya Muungano, suala hilo liliingizwa mwaka 1968, kwa kufuata taratibu husika, kama ambavyo sasa limeondolewa kwa njia na taratibu zilezile," alieleza Mchenga.

No comments:

Post a Comment