Friday, 18 November 2016
JPM AMWAGA WINO SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI 2016
RAIS Dk. John Magufuli ametia saini Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu.
Hivi karibuni, Bunge lilipitisha muswada huo kabla ya kupelekwa kwa Rais, kwa ajili ya kutiwa saini na kuwa sheria.
Muswada huo uliwasilishwa bungeni na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na kisha wabunge kuujadili kwa siku mbili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, ilisema Rais Magufuli alitia saini sheria hiyo juzi, iliyopitishwa na Bunge la 11 katika mkutano wake wa tano mjini Dodoma.
“Rais Magufuli amesaini sheria hiyo tarehe 16 Novemba, 2016,” alisema Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa.
Aidha, Dk. Magufuli amewapongeza wadau wote kwa kufanikisha kutungwa kwa sheria hiyo.
"Naamini kuwa sheria hii itasaidia kuboresha sekta ya habari kwa manufaa ya wanataaluma wenyewe na Taifa," alisema Rais Magufuli kupitia taarifa hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment